WAZEE wetu hawakukosea waliposema mjenga nchi ni mwananchi na mbomoa nchi pia ni mwananchi mwenye, hata hivyo kuna tofauti kubwa sana baina watu wa aina mbili hizi.

Kwa tafsiri yetu mjenga nchi ni mwananchi aliyezaliwa na kufunzwa uzalendo jinsi ya kuitumikia nchi ya watu wake, huku nafsi yake ikijikataza kuondokana na tamaa na kuweka mbele maslahi binafsi.

Mjenga nchi anatofautiana sana na mbomoa nchi, ambaye naye amefunzwa kila kitu kama mjenga nchi, lakini mafunzo aliyopewa huyaweka pembeni na badala yake tamaa za maisha na maslahi binafsi huweka mbele.

Kadiri siku zinavyosonga mbele ndipo jamii inaposhuhudia kuporomoka kwa kitu kinachoitwa uzalendo na kupotea kwa mapenzi na nchi kiasi cha kujiuliza kwanini yatokee haya.

Ukichunguza kwa makini unamkuta mfanyaji wa vitendo vilivyokosa uzalendo babu na babu zake, bibi na bibi zake wamezaliwa kukua, kufa na kuzikwa hapa hapa na kwamba hawana shaka dhidi ya uzawa wao.

Hatuelewi kitu gani hasa kinawasibu vijana wetu hadi kusababisha kukosa uzalendo na badala yake kuwa wahujumu wa mali za jamii, ikiwemo kujihusisha ubadhirifu, wizi, rushwa kutowajibika na hata kujumu mali za umma.

Vijana na wasichana wanapelekwa skuli hadi kufika vyuo vikuu na kufundishwa fani mbalimbali, lakini kwa bahati mbaya wakeshaajiriwa hutumia nafasi zo kwa maslahi binafsi, huku ndiko kukosa uzalendo.

Katika kujihalalishia uovu wao, baadhi yao wameunda semi walizozipa tafsiri potofu dhidi ya badahi ya mamlaka na taasisi hapa nchini, utasikiwa wakiziita ‘chukua chako mapema’, hii ni semi inayohamasisha wizi na ufisadi dhidi ya mali za umma.

Serikali imewaajiri na kuwaamini kuwa utaalamu walionao utaongeza ufanisi na kusukuma mbele maendeleo ya taasisi, lakini stashahada, shahada na utaalamu huwekwa pembeni na kinachoendelea ni uhujumu kwenda mbele.

Tumefikia pahala vijana wanaoajiriwa hawana subira, wanachotaka ni japo kwa kutumia njia za mkato, ilimradi baada ya miaka michache ajira aliyoipata iwe imeshamlipa.

Hatusemi kwa hizo ni ndoto mbaya, hapana, hizo ni ndoto njema kwa sababu hayo ndio maendeleo yenyewe, haiwekazani umezaliwa nyumba ya udongo ufe kwenye nyumba ya udogo.

Ila maendeleo ya mfanyakazi binafsi yapatikane kwa njia za halali sio wizi na uhujumu wa mali za umma, ambapo kwa wale wanaofanya hivi ndio wanaotufanya leo tukiuleze uzalendo wao uko wapi?

Tunafikiri umefika wakati tuanzishe somo la uzalendo, ambayo pamoja na mambo mengine yataambatana na mambo ya maadili, ili vijana wetu wanaochipukia wawe na mapenzi ya kweli na nchi yao.

Aidha tuurejeshe utaratibu wa kisheria ambao uliwalazimisha vijana kutoajiriwa kabla ya kupitia Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU), ambapo kiukweli jeshi hili limekuwa msaada mkubwa katika kuwajengea uzalendo vijana wetu.

Tuseme kweli wafanyakazi wengi waliojiriwa serikali ambao wamepitia JKU nidhamu na uzalendo wao ni tofauti sana na wengi ambao hivi sasa wamekuwa wakiajiriwa bila ya kupitia jeshini hapo.