BAMAKO, MALI

JUMUIYA ya kiuchumi ya mataifa ya afrika magharibi ECOWAS, imesema kwamba ina wasiwasi kwamba serikali ya mpito ya Mali haija piga hatua za kutosha kuelekea uchaguzi uliopangwa kufanyika Februari mwakani kama ilivyokubaliwa baada ya mapinduzi ya kijeshi mwaka uliopita.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, ECOWAS ilisema kwamba hali ya kurejea kwenye demokrasia nchini humo inafuatiliwa kwa karibu baada ya kupinduliwa kwa rais Ibrahim Boubacar Keita na hasa ikizingatiwa kwamba eneo la Afrika magharibi limeshuhudia mapinduzi mara nne.

Baada ya mapinduzi ya Mali, viongozi wa kijeshi wanaoshikilia madaraka walikuwa wakipata shinikizo kutoka kwa mataifa wanachama wa ECOWAS na kukubali kuitisha uchaguzi wa rais na bunge baada ya miezi 18.

Hata hivyo kuahirishwa mara kwa mara kwa tarehe ya uchaguzi, kuchelewesha kwa uandikishaji wa wapiga kura pamoja na pendekezo la katiba mpya ni masuala yanayotia wasiwasi.

Kipindi cha mpito nchini humo kilikumbwa na tatizo jengine mwezi Mei baada ya kanali aliyeongoza mapinduzi ya kwanza Assimi Goita kuamuru kukamatwa kwa rais wa mpito, wakati yeye mwenyewe akishikilia wadhifa huo.

ECOWAS ilielezea wasiwasi wake wakati wa kumalizika kwa ziara ya wajumbe wake nchini humo wakiongozwa na aliyekuwa rais wa Nigeria Goodluck Jonathan.

Serikali ya mpito hata hivyo iliahidi kuheshimu ahadi ya kuitisha uchaguzi, ingawa baadhi ya maofisa wanasema kwamba huenda isiheshimiwe.

Mchambuzi wa masuala ya siasa Bassirou Ben Doumbia alisema kwamba muda uliopo hautoshi kuitisha uchaguzi wenye hadhi.

Anasema kuwa iwapo mambo yataharakishwa, basi yatapelekea mizozo ya kawaida ambayo inajitokeza baada ya kila uchaguzi.