NA MOHAMMED SHARKSY, SUZA

HOMA ya uti wa mgongo ni ugonjwa hatari unaotokana na shambulizi la vimelea katika tando inayofunika uti wa mgongo na ubongo umeeingia DRC kwa kasi kubwa tatizo hili lisipodhibitiwa huweza kusababisha kifo.

Kutokana na wimbi la maumbikizi ya ugonjwa wa homa ya uti wa mgongo uliotokezea katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, ambapo inakisiwa kuwa watu wapatao 129 wameshafariki dunia na wengine 261 wakishukiwa kuambukizwa ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa  na Shirika la Afya  Ulimwenguni ( WHO) inasema idadi ya vifo vinavyoripotiwa kutokana na ugonjwa huo ni kubwa ikiwa ni uwiano wa asilimia 50.

Akizungumzia mlipuko huo Dk. Matshidiso Moeti, Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika amesema “Homa ya uti wa mgongo ni maambukizo mazito na ni changamoto kubwa kwa afya ya umma. Tunajitahidi kupambana nayo kwa kasi, tunatoa dawa na kupeleka wataalam kuunga mkono juhudi za serikali za kudhibiti mlipuko huo kwa muda mfupi zaidi.”

Aliongeza kuwa zaidi ya wagonjwa 100 tayari wanapata matibabu nyumbani na katika vituo vya afya huko Banalia. Homa ya uti wa mgongo huambukizwa miongoni mwa watu kupitia mate au makohozi yaliyotemwana watu walioambukizwa.

SERIKALI YA TANZANIA YATOWA TAMKO

Serikali ya Tanzania imewataka raia wake kuchukua tahadhari kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa homa ya uti wa mgongo uliotokea katika jimbo la Tshopo nchini DRC Congo.

Vimelea vya ugonjwa huu huambukizwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine kwa njia ya hewa au kukaa na mtu mwenye maambukizi, kulingana na wataalam wa magonjwa sugu ya maambukizi.

Mlipuko wa Homa ya uti wa mgongo ni tishio kwa sasa barani Afrika, kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa Septemba 8, 2021 na Shirika la Afya Duniani (WHO) kanda ya Afrika.

Taarifa iliyotolewa jana Alhamisi Septemba 16, 2021 na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Aifelo Sichwale, imesema ni vyema kuendelea kuchukua tahadhari kwani magonjwa hayana mipaka, hususani mikoa ya Tanzania inayopakana na DRC, ikiwemo Kigoma, Rukwa, Kagera, Katavi na Songwe.

“Ugonjwa huu huchukua siku mbili hadi 10 tangu kuambukizwa hadi kuanza kuonyesha dalili,” amesema, Dk.  Sichwale.

Kulingana na Shirika la Utanagzaji la nchini (BBC), Mganga mkuu wa serikali ya Tanzania Dk. Aifelo Sichwale amesema kuwa Wizara inaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa ugonjwa huo nchini DRC na kuchukua hatua ili kuzuia na kujiandaa kukabiliana na tishio la ugonjwa huo endapo utajitokeza nchini kama alivyozungumza na Martha Saranga.

DALILI NA ISHARA ZA HOMA YA UTI WA MGONGO

Joe David Kanumbar   Daktari na Muhadhiri kutoka Skuli ya Afya na Sayansi za Afya (SUZA) alisema dalili kuu za ugonjwa huu ni pamoja na kujihisi homa kali homa kali, maumivu makali ya kichwa, kutapika, dalili na viashiria vya uti wa mgongo ni pamoja na shingo, mwili kukakamaa na kuwa ngumu isivyo kawaida, kichefuchefu na kutapika, kupoteza fahamu na degedege.

kushindwa kuvumilia mwangaza (photophobia), kutoweza kukaa sehemu yenye makelele na kwa watoto utosi kuuma. Daktar Joe alisema kwamba kuna uchunguzi kwa jina la kitaalamu.

Wakati wa kumfanyia mgonjwa uchunguzi, daktari anaweza kuangalia pia viashiria vingine vinavyoonesha kuwapo kwa ugonjwa wa uti wa mgongo ikiwamo kukakamaa kwa shingo.

Mgonjwa hupata hisia za maumivu kwenye uti wa mgongo yanayozuia kukunjua goti wakati anapofanyiwa uchunguzi wa kukunjua goti lake.

Ishara hii hujulikana kitabibu kama ‘kerning’.

Wakati mwingine mgonjwa anapoelekezwa kujitahidi kukunja shingo, miguu (yaani paja pamoja na goti) navyo hujikunja, ishara hii hujulikana kitabibu kama Brudzinski.

Islam Haji Mwita, mhadhiri wa Skuli ya Afya na Sayansi za tiba ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), alisema kumekuwa kuna imani  potofu kutoka na uwelewa mdogo katika jamii kuhusu  mgonjwa  wa homa ya uti wa mgongo  kwamba anayepatwa ana degedege.

Alisema kwamba kuna baadhi ya watu wenye imani potofu wanaweza kuhusisha hali hii na mambo ya kishirikina ikiwamo kuvamiwa na mashetani au kurogwa.

Muhadhiri Islamu alisema kwamba ukweli ni kwamba, dalili na viashiria kama hivyo inaweza kuwa ni tatizo la kiafya ikiwamo homa ya uti wa mgongo ambayo kitabibu hujulikana kama Meningitis.

Kwa hivyo ametowa wito kwa jamii kuachana na fikra potofu kama hizo pamoja kuwapeleka wagonjwa wa aina  hii  hospital na  vituo vya afya kwa ajili ya uchunguzi na matibabu yanayo faa alisema.

Ni ugonjwa hatari unaotokana na shambulizi la vimelea katika tando inayofunika uti wa mgongo na ubongo, tatizo hili lisipodhibitiwa huweza kusababisha kifo mapema.

Huba Khamis Rashid, mhadhiri kutoka SUZA alisema kwamba watu walio katika hatari zaidi ya kupata ugonjwa huu ni pamoja na wagonjwa wenye kinga dhaifu ikiwamo wale wanaoishi na virusi vya UKIMWI.

Vilevile huwapata watu wanaoishi katika msongamano wa watu, watoto wadogo, wagonjwa waliokatika matibabu, wakimbizi katika kambi, wasafiri wa makundi na wanaofanya kazi katika maabara.

Vili vile Huba alisema homa hii huwa inasababishwa na makundi ya vimelea vya homa ya mapafu na Kifua Kikuu ambavyo mara kwa mara vimekuwa vinasababisha kujitokeza kwa magonjwa mbalimbali.

Virusi wanaosababisha homa hiyo ni pamoja na Herpes simplex aina ya 2, virusi vya ukimwi na virusi wanaosababisha mkanda wa jeshi.

Kwa upande wa vimelea vya fangasi ni pamoja na wale wajulikanao kama Coccoidiodomycosis na Cryptococci meningitides.

Homa hii inaposababishwa na bakteria, hatari ya kifo inakuwa kubwa zaidi na mara nyingi mgonjwa anapopona anaweza kupata ulemavu wa kudumu ikiwamo kupoteza uwezo wa kusikia, madhara katika ubongo na kuwa na udhaifu wa kujifunza.

NI VIPIMO GANI VINATUMIKA KATIKA UCHUNGUZI WA HOMA YA UTI WA MGONGO?

Ingawa uwepo wa viashiria na dalili vinaweza kumsaidia daktari kupata jawabu sahihi la ugonjwa, pia, anaweza kufanya vipimo vifuatavyo ili kuthibitisha kile alichokibaini.:

Kuchunguza damu ya mgonjwa kwa ajili ya kuangalia uwapo wa vimelea vinavyosababisha ugonjwa na kufahamu aina ya vimelea hivyo.

Damu inaweza pia kutumika kuotesha vimelea maabara ili kugundua aina ya vimelea na dawa gani nzuri zinazofaa kwa ajili ya matibabu (culture and sensitivity).

Kuchukua sampuli ya maji ya uti wa mgongo wa mgonjwa na kuyachunguza maabara ili kutambua uwapo wa vimelea, aina ya vimelea na dawa zinazofaa kutibu vimelea hao.

Kwa baadhi ya maeneo yenye vifaa kama CT-scan na MRI, mgonjwa pia huweza kuchunguzwa kwa kutumia vifaa hivi ili kufahamu uwapo wa ugonjwa, sehemu yalipo madhara yaliyosababishwa na ugonjwa huu.

Hata hivyo, vipimo hivi haviwezi kutambua aina wala dawa ya kutibu vimelea vinavyosababisha ugonjwa huo.

MATIBABU YA UGONJWA WA UTI WA MGONGO

Ugonjwa huu unatibika, ni vizuri mgonjwa mwenye dalili nilizotajwa afikishwe haraka katika huduma za afya na siyo kupelekwa kwa waganga wakienyeji kwa wale wenye imani potofu.

Huduma za kuhakikisha mgonjwa anapumua vizuri na njia ya hewa iko salama hutolewa katika huduma za afya.

Dawa za homa na kuangamiza vimelea waliosababisha homa hii hutolewa.

NINI MADHARA YA HOMA YA UTI WA MGONGO?

Homa ya uti wa mgongo inaweza kusababisha kuamshwa kwa chembechembe za damu zinazosababisha damu kuganda kitaalamu – Disseminated Intravascular Coagulopathy (DIC).

Kuvuja damu kwa katika tezi za Adrenalin na kusababisha kutokea kwa ugonjwa ambao kitabibu hujulikana kama waterhouse friderichsen syndrome.

Homa hii ni moja ya chanzo cha kujitokeza tatizo la kujaa maji kichwani (hydrocephalus) kwa watoto.

Madhara mabaya ni yale ya kudumu ikiwamo kupoteza uwezo wa kusikia na kuwa na uwezo mdogo wa kujifunza.