NA MOHAMMED SHARKSY, SUZA

KILA ifikapo Septemba 29 ya kila mwaka dunia huadhimisha siku ya moyo, ambapo wadau wa masuala ya afya wakiratibiwa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) hutumia kama jukwaa la kuhamasisha kuhusu magonjwa ya moyo.

Ujumbe wa maadhimisho ya mwaka huu unalenga katika elimu kwa umma kwamba Moyo ni kitovu cha kila kitu yaani afya ambayo ndiyo uzima wa mwanadamu, ambapo WHO inataka jamii ifahamu kuwa moyo ukipata matunzo muruwa afya huwa sawia.

Katika chapisho la shirika hilo linaelekeza ulaji unaozingatia kanuni za afya, kupunguza matumizi ya bidhaa za ulevi kama pombe na sigara na ufanyaji mazoezi kama njia ya kuepuka magonjwa ya moyo.

Kwa mujibu wa WHO, zaidi ya watu milioni 17 hufariki dunia kila mwaka kutokana na magonjwa ya moyo, wengi wao huwa ni watumiaji wa bidhaa zinazotokana na tumbaku, kula vyakula vyenye chumvi nyingi na kutofanya mazoezi.

WHO linaeleza kuwa wengi wanaweza kuokolewa kwa kupatiwa tiba za shinikizo la damu, shinikizo la lehemu na mengine yanayosababisha magonjwa ya moyo na kiharusi.

Kiafya moyo unatakiwa kuwa na mapigo takribani 70 mpaka 72 kwa dakika kwa mtu ambaye kiafya hana tatizo lolote, hali hii huwa inatokea mara chache kwa muda na kutoweka kutokana na sababu chache kama vile uoga na hasira.

Shambulizi la moyo (heart attack) hutokea pindi tu mtiririko wa damu kuelekea kwenye misuli ya moyo unapokatishwa. Ikiwa mtiririko wa damu haukurejeshwa haraka misuli ya moyo inaweza kuharibika na hatakufa kutokana na ukosefu wa oksijeni.

Shambulio la moyo ni hali ambayo mishipa midogo hujifunga kuzuia damu yenye utajiri wa oksijeni kufikia moyo. Hii husababisha kifo cha tishu hizo za moyo, ambazo hutolewa na mishipa iliyofunikwa. Katika kesi ya kuchelewesha matibabu, mtu huyo anaweza kupata mshtuko wa moyo.

DALILI NA ISHARA ZA SHAMBULIO LA MOYO

Mhadhiri kutoka Skuli ya Afya na Sayansi za Tiba katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Dk. Huba Khamis Rashid alisema kuna umuhimu mkubwa wa kujua dalili za mshtuko wa moyo ambazo huambatana na:

Kujisikia vibaya kifuani, kifua kubana au kuuma. Dalili ya kawaida ya shambulio la moyo ni maumivu ya kifua au kuijisikia vibaya. Shambulio la moyo husababisha maumivu katikati ya kifua kwa dakika chache na kisha kutoweka, maumivu haya yanaweza kurejea tena baada ya muda kidogo.

Mgonjwa hujisikia kama anakandamizwa kifuani, anabanwa na wakati mwingine huhisi mauamivu makali au ya kadri. Wakati mwingine maumivu yanayosababishwa na shambulio la moyo hufanana na yale ya kuvimbiwa au kiungulia.

Dk. Huba   aliendelea kwa kusema kwamba kupumua kwa shida ambapo mara nyingi hutokea kabla mgonjwa hajaanza kujisikia vibaya kifuani, kujisikia vibaya kwenye mkono mmoja au mikono yote, mgongo, shingo, taya, au tumbo.

Dalili nyengine ni pamoja na kujisikia kichefuchefu, kutapika, kizunguzungu na kutokwa na jasho.

Dk. Huba alisema sio mashambulizi yote ya moyo huanza ghafla na kusababisha maumivu makali kifuani . Ishara na dalili za shambulio la moyo hazifanani kwa kila mtu, ambapo mashambulizi mengi ya moyo huanza polepole kama maumivu ya kawaida au kujisikia vibaya tu. Watu wengine hawana dalili kabisa (hii inaitwa shambulio la moyo la kimyakimya).

 

SABABU ZA SHAMBULIO LA MOYO

Mshituko wa moyo hutokea mara nyingi kama matokeo ya magonjwa yanayoathiri ateri za moyo. Ugonjwa unaoathiri ateri za moyo husababishwa na utando wa mafuta ambao hujengeka taratibu.

 

kwa miaka mingi ndani ya ateri za moyo (ateri hizi ndizo hutiririsha damu na oksijeni kwenye moyo), hatima yake ni kuwa sehemu ya ateri yenye utando mwingi huchanika na kusababisha damu kuganda juu ya utando. Kama donge la damu iliyoganda litakua na kuwa kubwa sana, litaziba kabisa ateri na kuzuia mtiririsho wa damu yenye oksijeni kufika kwenye misuli ya moyo

 

SABABU ZINAZOONGEZA HATARI YA SHAMBULIO 

Uvutaji uliokithiri wa sigara, shinikizo la juu la damu, kiwango kikubwa cha mafuta (cholesterol) kwenye damu, kuongezeka kwa  uzito wa mwili, kitambi, kutofanya mazoezi, kisukari na umri.

Hatari ya kupata shambulio huongezeka mara dufu kwa wanaume wenye miaka zaidi ya 45 na kwa wanawake wenye umri wa miaka zaidi ya 55.

Kuwepo kwa historia ya kupata magonjwa ya ateri za moyo kwenye familia ya mtu kunaongeza maradufu hatari ya kupata mshtuko, hatari huongezeka zaidi kama baba au kaka yako aligundulika kuwa na ugonjwa wa ateri za moyo kabla ya miaka 55,au ikiwa mama au dada yako amegunduliwa kuwa na ugonjwa wa ateri za moyo kabla ya miaka 65.

WATU WALIO KATIKA HATARI YA KUPATA SHAMBULIZI LA MOYO 

Dk. Joe David Kanumbar  Muhadhiri kutoka Skuli ya Afya na Sayansi za Tiba (SUZA) alisema watu walio katika hatari ya kukumbwa na ugonjwa huu ni pamoja na wenye umri mkubwa miaka 45 kwa wanaume na 55 kwa wanawake.

Wavuta sigara, watu wenye mafuta ya lehemu katika damu au wale wenye mafuta mabaya aina ya ‘triglycerides’ na ‘low density lipoprotein’ kwa kiwango kikubwa katika damu zao.

Wenye ugonjwa wa kisukari, wenye matatizo ya shinikizo la damu, walio na unene kupita kiasi, wenye matatizo sugu ya kushindwa kufanya kazi kwa figo zao, wanywaji wa pombe kupindukia, watumiaji wa dawa za kulevya hasa ‘cocaine’ na ‘methamphetamine’.

Watu wenye msongo wa mawazo na watu wenye upungufu wa vitamin b2, b6, b12 na folic acid. daktar Joe aliwashauri watu wenye matatizo kama hayo ni vizuri kumuona muhudumu wa afya mapema iwezekanavyo.

VIPIMO NA UCHUNGUZI WA SHAMBULIO LA MOYO

ECG – Kipimo hiki huonyesha ni sehemu gani ya moyo iliyoathirika, Coronary angiography kipimo chenye kusaidia kwa kuangalia wapi ambapo mishipa ya damu imekuwa membamba sana kupita kiasi au imeziba.

Kipimo chengine ni Cardiac markers levels, X-ray ya kifua (chest X-ray), MPI (Myocardial Perfusion Imaging) – Kipimo hiki hufanywa kwa kutumia mashine maalum ya PET Scan ambapo kinauwezo wa kugundua tatizo la shambulizi la moyo.

huchunguza kikamilifu maumivu ya kifua, huangalia mwelekeo wa tiba ya kuzuia damu kuganda, hutoa mwelekeo wa ugonjwa wa shambulizi la moyo kama ni mzuri au mbaya, hutathmini ubora wa tiba ya shambulizi la moyo kabla na baada ya mgonjwa kupata tiba, huweza kutambua hata shambulizi la moyo ambalo si rahisi kugundulika kwa kutumia vipimo vyengine na pia hutathmini ukubwa wa tatizo la shambulizi la moyo. Hata hivyo kwa sasa kipimo hiki hakipatikani nchini kwetu.

Ili kuweza kutambua uwepo wa tatizo hili, mwaka 1979, shirika la Afya Duniani (WHO) liliweka vigezo vya kutambua shambulizi la moyo. Vigezo hivyo ni historia ya kuwa na maumivu ya kifua zaidi ya dakika 20, mabadiliko katika kipimo cha ECG na kupanda na kushuka kwa kipimo kiitwacho kitaalamu cardiac biomarkers hasa creatine kinase – MB na troponin.

HATUA GANI ZA HARAKA ZINAPASWA ZINAZOCHUKULIWA

Kufuatia mambo lazima izingatiwe wakati mtu anampata mtu aliye na dalili zilizotajwa hapo awali: kutambua dalili, piga simu nambari ya dharura kufikia hospitali iliyo karibu, ikiwezekana kutafuna na kumeza asipirini. Tafadhali angalia kuwa wewe sio mzio wa aspirini.

Chukua nitroglycerine, ikiwa daktari wako amekuamuru hapo awali, ikiwa uko na mtu huyo kupata mshtuko wa moyo, unaweza kuanza ufufuaji wa moyo na moyo.

MATIBABU YA SHAMBULIO LA MOYO

Shambulio la moyo ni tatizo linalohitaji matibabu ya dharua. Lisipotibiwa kwa haraka husababisha kifo katika muda mfupi sana tangu mgonjwa apatwe na tatizo. Matibabu ya tatizo hili hujumuisha

Kumpa mgonjwa hewa ya oksijeni, mgonjwa hupewa vidonge vya aspirini ndogo kuzuia damu kuganda (thrombolytic) kwa ajili ya kuyeyusha damu iliyaganda na hivyo kuzibua mirija midogo ya damu katika moyo iliyozibwa na kuganda huku kwa damu.

Vile vile mgonjwa hupewa dawa za kuweka chini ya ulimi kiitwacho nitrogylycerin (glyceryl trinitrate) ambazo husaidia kutanua mishipa ya damu (vasodilation).

Dawa ya kutuliza maumivu kwa mfano morphine, dawa ya kuyeyusha mafuta katika mishipa ya damu kama vile clopidogrel, kuzibua mishipa ya damu inayosambaza damu katika moyo kwa kutumia – Percutaneous coronary intervention (PCI) na upasuaji (CABG)

NJIA ZA KUZUIA SHAMBULIZI LA MOYO

Kuacha kuvuta sigara Kupunguza mafuta na chumvi kwenye mlo na kuongeza matunda na mboga mboga. Mabadiliko haya yanaweza kusaidia kupunguza shinikizo la damu na mafuta kwenye damu.

Kupunguza uzito, kuacha uvutaji sigara, kufanya mazoezi ya mwili huimarisha misuli ya moyo. Muulize daktari wako kiasi gani na aina gani ya mazoezi, moyo na mwili unaweza kuhimili.

Kufanya mazoezi ya mara kwa mara, kupunguza unywaji wa pombe, kubadilisha aina ya mlo. Kupunguza mafuta katika mlo na chumvi na kuna utafiti unaosema kuwa uchangiaji damu hupunguza hatari ya magonjwa ya moyo hasa kwa wanaume.

MADHARA YA SHAMBULIZI LA MOYO

Moyo kushindwa kufanya kazi (heart failure), matatizo katika mfumo wa mapigo ya moyo (Atrial fibrillation) ambayo hatimaye hupelekea kifo, shambulizi la moyo kurudia mara ya pili na kifo cha ghafla (sudden death).