KAMPALA, UGANDA

RAIS wa Uganda Yoweri Museveni amesema kuwa, nchi yake iko tayari kutuma wanajeshi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa ajili ya kukabiliana na waasi wa ADF endapo serikali ya Kinshasa itatoa ridhaa ya hilo.

Rais Museveni alibainisha kuwa, majadiliano yanaendelea na mwenzake wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Félix Tshisekedi.

Alipoulizwa kuhusu ugaidi nchini Msumbiji, Rais Museveni alisema kuwa, chanzo cha tatizo hilo kiko kwa jirani yake Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Pia alisema tatizo la Msumbiji linahusiana na tatizo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Magaidi hawa nchini Msumbiji walipitia DRC katika kipindi cha miaka ishirini iliyopita.

Tatizo la DRC lazima litatuliwe kwa pamoja na lile la Msumbiji na kusema kuwa wako tayari kutoa msaada wakati wowote kwa ajili ya kukabiliana na waasi wa ADF huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Kundi la waasi wa ADF linalotokea kaskazini mashariki mwa Uganda limekuwa likiendesha shughuli zake za ugaidi katika maeneo ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo tangu muongo wa 90, ambapo limeua mamia ya watu, mbali na kupelekea malaki ya wengine kuwa wakimbizi.

Eneo la mashariki mwa Jamhuuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) limekuwa likishuhudia machafuko ya mara kwa mara baina ya makundi ya wanamgambo kwa upande mmoja na wanamgambo na maofisa usalama kwa upande mwengine, kutokana na kuwa na utajiri mkubwa wa madini hususan dhahabu na almasi.