NA LAYLAT KHALFAN

IKIWA ugonjwa wa corona unaendelea kusumbua duniani, Zanzibar kama sehemu ya dunia nayo imekuwa na wagonjwa wa ugonjwa huo hasa katika wimbi hili la tatu.

Hivi karibuni Waziri wa Afya, Ustawi wa jamii, jinsia na watoto Nassor Ahmeid Mazrui, alisema kuwa hadi sasa ugonjwa huo umeshauwa watu wapatao 40 na wengine zaidi ya 30 wako katika uangalizi maalumu huku walioambukizwa wakifika 300 kati ya hao wamo wageni zaidi ya 200 na wengi wao wamepona.

Alisema ugonjwa wa corona Zanzibar upo na kwamba jamii inapaswa kuchukua tahadhari ya kujikinga na ugonjwa huo.

Katika makala haya itazungumzia namna ya baadhi ya wafanyabiashara waliopoteza kazi zao kutokana na ugonjwa wa corona hasa ule wa wimbi la kwanza na la pili.

Miongoni mwa biashara hizo ni pamoja na nguo za mitumba, kazi za daladala ambazo ziliathiriwa na janga la virusi vya corona na kusababisha baadhi ya wamiliki wa magari, wasimamizi wa magari na wazalishaji wa viwanda mbalimbali kushuka kiuchumi.

Wakizungumza na Makala haya kwa nyakati tofauti na baadhi ya wafanyabiashara wa nguo za mitumba, walisema biashara imekuwa ngumu kwasababu kuna baadhi ya watu walikuwa na imani kuwa nguo hizo zinaleta ugonjwa wa corona.

Aidha walisema kuwa baadhi ya watu wameacha kabisa kutembelea maeneo yanayouzwa nguo za mitumba kwa mdai kuwa nguo hizo ni za watu waliokufa kwa corona.

Mmoja kati ya wafanyabiashara hao anaejulikana kwa jina la umarufu Mwarabu anaemiliki duka la mitumba maeneo ya Darajani tobo la pili, anasema hali ya biashara hairidhishi kutokana na watu wengi kuhofia kuathirika kwa ugonjwa huo.

“Nyakati kama hizi nimezongewa kiasi ambacho sipati hata kukohoa ama kutema mate pembeni watu walivozunguka na kufurika kwa kukimbilia bidhaa hii, lakini kwasasa hali bado haijarudia katika uhalisia wake”, anasema.

Anasema kwa hafla ukifika katika eneo hilo utajiuliza hapa kunatolewa sadaka ama kuna sherehe Fulani inafanyika kutokana na wingi wa watu kumbe ni wateja wananunua bidhaa hiyo.

Mwarabu anasema tangu kuanza kwa ugonjwa huo wateja wengi wanasema nguo zinazotoka nje zinatoka kwa wale waliouguwa ugonjwa huo hivyo na wao waliogopa kupata virusi hivyo jambo ambalo wanahofia kuambukizwa.

“Baada ya kuona hali ishakuwa ngumu huku watoto nyumbani wanataka kula tulilazimika wafanyabiashara wote kujikusanya pamoja na tukatafuta mbinu mpya ya kuuza nguo zetu kupitia mitandao ya kidigitali”, anasema Mwarabu.

Kwa upande wake mfanyabiashara maarufu wa bidhaa hiyo, Farhin Kisule, alisema tangu kuanza kwa corona biashara yake inasua sua wateja wanakuja kwa kunyatia nyatia huku wakiamini wakinunua nguo hizo watapata maambukizi ya virusi vya corona.

“Nilizoea kuuza karibu mzigo wote kwa siku huku wateja wengine wakikosa bidhaa hiyo, lakini hivi sasa kwa siku naweza kupata wateja wawili mpaka watano”, anasema.

Amina Hassan mfanyabishara wa vitu mchanganyiko wa bidhaa za mitumba, anaefanya shughuli zake Kikwajuni Jijini Zanzibar, anasema katika kipindi cha corona kwa kiasi kikubwa biashara yake ilipungua na kupelekea soko lake kufa kwa kipindi hicho.

Anasema asilimia 50 ya wateja wake walikata kabisa huku akiwa anasubiri wateja wake kuanzia asubuhi hadi jioni lakini cha ajabu haambulii kitu, walikuwa wakipita eneo hilo na kupaona kama kituo cha polisi.

“Kutokana na hali hiyo tukawa tunaweka mikakati ya kudumisha masharti ya kuweka maji ya kunawa kwa sabuni, sanitaizer barakoa lakini hali haikusaidia kitu kwani wateja walikuwa hawaamini kabisa na kuamini kuwa wanaweza kuambukizika tu ugonjwa huo kupitia bidhaa zetu”, anasema mfanyabiashara huyo.

Kwa upande wake Hassan Ramadhan Pele, Mfanyabishara wa mabaibui, katika maeneo ya Mwanakwerekwe, anasema ndani ya kipindi hicho mwamko wa wateja ulikua mbaya kwani wengi wao walikua hawendi kupata mahitaji yao hapo kwa kuhofia corona.

“Athari kubwa kiufupi ndio hiyo kwasababu nilikuwa naenda kazini na kurudi nyumbani bila ya mafanikio yoyote labda kupata pesa ya mboga tu”, anasema Hassan.

Aidha, anasema alikuwa haruhusu kwenye biashara yake wateja kuingia bila ya kuvaa barakoa kwa kuhofia kusambaa maradhi hayo kwa hiyo nayo pia iliwakimbiza wateja.

“Kiufupi mabaibui yapo vizuri na yanapigwa dawa na ya kija muonekano wake unayaona na kama hayakupigwa yanaojuilikana kwasababu muonekano wake ni mbaya kwaiyo mzigo kama huo tunaukataa”, anasema mfanyabiashara huyo.

Alisema hajawahi kupata mzigo wenye shaka katika mizigo anayoagiza kwasababu kama kuathirika ama kufa angeanza yeye kutokana na kuwa ni biashara anayofanya miaka mengi sasa.

Sambamba na hayo wafanyabiashara hao waliwataka wanunuzi wa bidhaa hiyo kuondoa shaka na badala yake walitakiwa kuiamini biashara hiyo kwani ipo salama kwa afya zao.

WANAVYOZUNGUMZA WANUNUZI WA MITUMBA

Nao wanunuzi ama wateja wa bidhaa hiyo, walisema kwa sasa hawana imani na bidhaa itokanayo na mitumba kwa kuhofia kupata maradhi ya corona.

“Mimi ni miongoni mwa washabiki wa bidhaa hii maarufu lakini niliposikia kuwa nguo zinazovuliwa maiti wenye ugonjwa huo ndizo zinazosafirishwa na kuuziwa sie basi mpaka leo siamini kabisa kununua bidhaa hiyo”, anasema Mwanaisha Haji Ussi, mkaazi wa Fuoni Mambo sasa Wilaya ya Magharibi ‘B’ Unguja.

Kwa upande wake Mwangalizi wa Wafanyakazi katika kampuni ya Savannah International (Z) Limited, Fikirini Amani Khalfan, anasema katika kipindi cha corona kampuni hiyo ilitetereka kiuchumi kwani hawakupata bidhaa nyingi kutoka nje na kupelekea kiwango cha uzalishaji kupungua.

“Uingizaji wa mzigo ulipungua sana na kusababisha kampuni yetu kupata hasara kubwa na kushindwa kumudu hali hiyo kwa baadhi ya wafanyakazi wetu”, anasema.

Fikirini anasema kikawaida walikuwa wanaingiza mzigo hadi kontena 10 lakini kipindi cha corona mambo yalikuwa mabaya na kushuka hadi kontena nne kwa mwezi mzima.

Aidha, anafahamisha kuwa, kutokana na hali hiyo kampuni ililazimika kupunguza vibarua waliokuwa hawana mkataba na kuwapa likizo za kawaida wafanyakazi wenye mkataba wasiopungua wanane.

“Wafanyakazi wetu wapo 115 kati ya hawa 17 tukawapunguza kutoendelea na kazi kutokana na kumudu kuwalipa na wafanyakazi wetu ambao wanamkataba tukawapa likizo hdi pale hali itakaporuhusu”, anasema.

Anasema kampuni yake inafuata masharti uliowekawa na serikali na kupanga utaratibu malum wa kuwapeleka wafanyakazi wao hospitali kufanyiwa vipimo kila baada ya miezi sita kwa kuchunguzwa maradhi mbalimbali kwa ajili ya afya zao.

BIASHARA YA USAFIRISHAJI ABIRIA (DALADALA)

Usafiri wa umma Zanzibar

Kwa upande wa wafanyabiashara wa daladala walisema wimbi la kwanza la ugonjwa wa corona liliathiri sana biashara ya usafirishaji abiria daladala.

“Kwa kuwa serikali ilikataza na kuzuia safari zilizokuwa hazina ulazima ili kudhibiti maambukizi ya maradhi hayo kuendelea kuenea nchini, biashara hiyo ilikuwa katika wakati mgumu kiasi ambacho walishindwa kuendesha maisha yetu”, alisema.

Walisema wateja wao wakubwa walikuwa ni wanafunzi wa vyuo, wafanyakazi, watalii wanafunzi wa madrasa, lakini kutokana na amri hiyo walikosa wateja kwani karibu taasisi zote zilifungwa kwa hofu hiyo.

Mmoja kati ya madereva hao, Issa Machano Haidari, ni dereva wa gari za abiria njia ya Fuoni, anaiambia Makala hii kuwa katika kipindi cha corona biashara ilikua ngumu abiria walikua hamna kwa kuhofia kuambukizwa maradhi ya corona.

“Jambo kubwa lililotuathiri ni hili la kufungwa kwa skuli, vyuo vikuu, madrasa baadhi ya sekta kufungwa kabisa kama vile utalii, wakati hao sisi ndio waliokuwa wateja wetu wakubwa wanaotuingizia kipato chetu cha kila siku.

Kwa upande wake dereva wa gari zinazoenda Kitope Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja, Said Abdul Shakur Mfaume, anasema katika kipindi cha corona kazi ilikuwa mbaya kiasi ambacho ilipelekea hadi kulaza gari yake na kutafuta shughuli nyengine za kufanya kwa lengo la kujipatia kipato.

Anasema kikawaida alikuwa anapata kodi ya kupeleka watu kwenye sehemu mbalimbali ikiwemo sherehe za harusi, maziko, mikutano, lakini kipindi hicho walikosa kodi hizo kwa kuwa serikali ilishapiga marufuku mkusanyiko ya watu.

“Kwa kawaida kwa siku alizoea kupata zaidi ya shilingi 150, 000 lakini kipindi hicho ilikuwa ni ngumu kupata hata shilingi 100,000 kwa siku na kukatisha ndoto

Nae Hafidh Machano Ameir, mwendesha gari za Makunduchi, anasema katika kipindi cha corona aliamua kuacha kazi hii nakutafuta kazi nyengine kwa kuwa ilikuwa haimkidhi haja.

“Nilizoea kwa siku kwenda ruti zaidi ya tatu kutoka shamba hadi mjini lakini kipindi hichi kwa siku naenda ruti kama mbili hazizidi ukiangalia ninafamilia inanisubiri kutoa huduma”, anasema.

Dereva wa gari za Nungwi, Khamis Makame, alisema katika kipindi cha corona hali ilikuwa mbaya kwani kikawaida alikuwa anakusanya zaidi ya shilingi 300,000 kwa siku lakini ugonjwa wa corona umeteteresha uchumi na kushuka hadi shilingi 150,000.

“Gari ya watu 30 kipindi hichi unaruhusiwa kupakia watu 20, gari ya watu 25 unaruhusiwa kupakia watu 16 na hvyo hufiki salama abiria akiwa anatiliwa shaka anashushwa kwaiyo idadi inazidi kupungua na kipato kinazidi kushuka”, anasema.

Kwa upande wa Wamiliki wa magari hayo, walisema katika kipind hicho mambo yalikuwa magumu kwa kuwa kazi zililala.

Walisema wamezoea kupokea kwa siku zaidi ya shilingi 50,000 wengine hadi 70,000 kwa kila jua linapotua kulinganisha na njia Fulani lakini kwa bahati mbaya mambo yalikwenda songombingo na ikiwa kipato wanachopata hakitambulikani.

Mohammed Issa Kitwana, Mmiliki wa gari, anasema kipindi hicho mambo yalikuwa magumu maana gari yake imelala mapema saa 4:00 za usiku lakini toka kuanza kwa ugonjwa huo, saa 12 jioni gari imo ndani.

Kwa upande wa Wasimamizi wa gari za Shamba (MABAGUANI), walisema katika kipindi cha corona hali kiuchumi ilitetereka kwasababu baadhi ya wadau wa magari waliwakosa kutokana na biashara hiyo ilikua ngumu na kuamua kutafuta kazi nyengine kwa ajili ya kupata riski huku nawao hali zao zikiendelea kuteketea.

Walisema katika kipindi hicho kipato chao kilishuka kwa asilimia 80 kutokana na kipato chao walichokuwa wakikipata hapo awali.

Moja kati ya wasimamizi hao, Adib Hassan Haji, alisema ili kipato chao kinyanyuke ni lazima wenye magari wapakie abiria wa kutosha ndipo nawao wanaweza kujikimu kipato chao cha kila siku.

Anasema mambo hayakuwa hivyo walivyozoea kwa kuwa madereva wengi wanategemea abiria wa kigeni hali ziliendelea kudhoofika na kukosa muelekeo mzuri wa kujiendeleza kimaisha.

Hivyo ndivyo namna corona ilivyosababisha athari kubwa katika biashara jambo ambalo watu wengi wameyumba kiuchumi kutegemea na biashara wanazofanya.