LONDON, UINGEREZA

SHIRIKA la kukabiliana na kudhibiti magonjwa la barani Afrika, Afrika CDC limeonya kwamba hatua ya Uingereza ya kuweka vizuizi vya usafiri kukabiliana na janga la virusi vya Corona, inaweza kuwafanya watu kote barani Afrika kuacha kudungwa chanjo.

John Nkengasong mkuu wa shirika hilo alisema ikiwa bara hilo linatumiwa chanjo halafu linaambiwa chanjo hizo hazitambuliwi, ujumbe huo unatowa changamoto kubwa kwa Afrika.

Uingereza chini ya hatua zake za vizuizi, imetangaza kutotambua chanjo kadhaa zilizotolewa katika nchi chache za Afrika.

Nchi hiyo haitambui chanjo zilizotolewa katika nchi nyingi za duniani na kote Afrika hata ikiwa chanjo hiyo imetokea Uingereza.

Akizungumza katika mkutano wa kila wiki na waandishi habari, Nkengasong alisema ujumbe huo wa Uingereza unasababisha mkanganyiko miongoni kwa watu wa bara la Afrika na kuwafanya wengi kutokwenda kuchanja.