BERLIN, JERUMANI
WIZARA ya mambo ya nje ya Ujerumani imeinyoshea kidole cha lawama Urusi kuhusiana na jaribio la kutaka kuiba data kutoka kwa wabunge.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani Andrea Sasse alisema nchi hiyo inashuku hayo ni maandalizi ya Urusi kutaka kusambaza habari za uongo kuhusu uchaguzi wa Ujerumani utakaofanyika baadaye mwezi huu.
Sasse alisema kuelekea uchaguzi huo kumekuwa na majaribio ya kupata data binafsi za wabunge wa shirikisho na majimbo kwa lengo la wizi.
Katikati ya mwezi Julai mkuu wa ujasusi wa ndani nchini Ujerumani alisema shirika lake liliona vitendo visivyo vya kawaida vya majaribio ya kupata taarifa kuhusu barua pepe za wabunge wa Ujerumani.