LUSAKA, ZAMBIA

SHIRIKA la Afya Duniani (WHO) limesema Afrika inakabiliwa na upungufu wa dozi milioni 470 za chanjo ya Covid-19 mwaka huu, baada ya mpango wa kimataifa wa Covax kupunguza makisio ya shehena yake, na kuibua wasiwasi wa aina mpya na hatari za kirusi hicho.

Kitengo cha WHO barani humo kilisema katika mkutano wa kila wiki mjini Brazaville, kwamba ni asilimia 17 tu ya wakaazi wa bara hilo ndiyo watakuwa wamechanjwa ikifikia mwishoni mwa mwaka huu, ikilinganishwa na shabaha ya asilimia 40 iliyowekwa na WHO.

Mkurugenzi wa WHO Afrika, Matshidiso Moeti, alisema ukosefu wa usawa na upatikanaji hafifu wa chanjo vinatishia kuyageuza maeneo barani Afrika, kuwa maeneo ya kuzalisha virusi visivyosikia chanjo.

Kutokana na uhaba wa kimataifa, mpango wa Covax utasafirisha karibu pungufu ya dozi milioni 150 kuliko ilivyopangwa.

Upunguzaji huu wa malengo ya chanjo unakuja wakati Afrika imevuka mambukizo milioni nane wiki hii,ilisema WHO.