NA MARYAM HASSAN

KIJIJI cha Matemwe Kigomani kilichopo wilaya ya Kaskazini ‘A’, kina wakaazi wapatao 4,549 kati ya hao wanaume 1,940 na wanawake 2,409.

Wakaazi hao wamezungukwa na rasilimali mbali mbali ikiwemo bahari na msitu ambazo huzitumika kwa shughuli mbali mbali za kiuchumi kwa kujiingizia kipato.

Lakini mbali na rasilimali hizo wamekuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa ya huduma muhimu ya vyoo.

Makala haya itazungumzia namna wanawake wa kijiji hicho wanavyoitumia rasilimali bahari na msitu kwa ajili ya kupata huduma hiyo.

Mwajuma Ali Makame ni mkaazi wa kijiji hicho anasema maisha yake yote tokea anazaliwa hadi sasa anafanya huduma yake katika fukwe.

Alieleza kuwa sababu kubwa ni kukosa uwezo wa kuchimba choo ambacho kinagharama kubwa na yeye hana uwezo wa kufanya hayo.

Anaeleza kuwa licha ya kupata maradhi mbali mbali lakini bado anaendelea kutumia fukwe na msitu kama ndio sehemu ya kufanya haja zake.

Dawa Juma Ame anaeleza kuwa tayari kamati mbali mbali zinawashajihisha kujenga vyoo lakini wanashindwa kwa sababu hawana uwezo wa kuchimba vyoo.

“Mimi tokea nipo mdogo najisaidia msituni na kwenye fukwe hadi sasa nishazaa nna watoto nao wanaenda huko huko kwa sababu sina uwezo wa kuchimba choo, la kama atatokea mhisani nipo tayari kunisaidia” alisema.

Anaeleza kuwa katika shehiya yao wanao viongozi wao lakini hawatakuwa na uwezo wa kumjengea choo mwananchi mmoja mmoja na badala yake watajikita katika huduma nyengine za kijamii.

“Naona shida kwenda msituni kwenda kujisaidia lakini nitafanyaje na sina uwezo mimi”, alisema Dawa.

Hata hivyo wamewaomba wahisani na watu wenye uwezo kuwasaidia kwa kuwachimbia vyoo ili kuondokana na kero ya kuendelea kujisaidia kwenye vichaka na pembezoni mwa fukwe za bahari.

Kombo Tano Juma, mkaazi wa kijiji hicho alisema wananchi wengi wa kijiji hicho wanashindwa kutumia matundu ya shimo kutokana na uwezo wao kuwa mdogo.

Alisema hali hiyo imewasababisha kuendelea kujisaidia sehemu zisizo rasmin kama vichakani na maeneo ya fukwe kila wanapotaka kwenda haja kubwa.

Nae Tatu Othmani Juma Kweri wa kijiji hicho alisema wanashindwa kufikia lengo la serikali la wananchi wa vijijini kutumia vyoo kutokana na kushindwa kumudu gharama za uchimbaji wa mashimo sambamba na kuwa ardhi yao kuwa ngumu kwa kuwa ukanda wao umezungukwa na mawe, jambo ambalo linawapa ugumu wachimbaji wa mashimo hayo.

“Uwezo wetu mdogo mno wa kuchimba mashimo ya vyoo tunataka tufanye hivyo kutimiza malengo ya serikali ya wananchi kutumia vyoo lakini wengi wetu kwenye kijiji hichi ni masikini”, alisema.

Sambamba na hayo aliwaomba watu wenye uwezo kuwasaidia ili kuondokana na tatizo hilo.

“Ukifika wakati wa kipindi cha mvua tunawasiwasi wa kupata maradhi ya mripuko kutokana na wengi wetu kuwa maskini, na maradhi husababishwa na mvua na majimaji, tunawaomba wahisani wajitokeze kutusaidia”, alisema.

Katika kulitafutia ufumbuzi suala hilo mwandishi wa makala haya alizungumza na Sheha wa Shehiya hiyo Tamo Ame Haji, kutaka kujua hatua gani alizochokuwa katika kutatua tatizo hilo, anaeleza kwamba alichukua jihudi ya kuzungumza na wananchi wake juu ya umuhimu wa matumizi ya vyoo.

Anaeleza kuwa baadhi ya wananchi walisema kwamba hawakati kuchimba vyoo lakini hawana uwezo.

Hatua kubwa aliyoichukua ni kufanya mjumuisho wa nyumba ambazo hazina vyoo na kupeleka serikalini na ahadi aliyopewa kuwa yatafanyiwa kazi.

Tano anaeleza kuwa katika shehiya hiyo nyumba zenye vyoo ni 348 na ambazo hazina vyoo ni 587, idadi hii ni kubwa kwa wale ambao hawana huduma hii.

“Kwa kweli sijachoka kufatilia kwa sababu ni suala muhimu na tokea niwasilishe matatizo hayo ni mwaka mmoja na nusu tokea mimi kuchaguliwa kuwa sheha na naendelea kufatilia”, alisema.

Sheha huyo aliiomba serikali kulitilia mkazo suala la huduma ya vyoo kwa kulifanyia kazi haraka ipasavyyo.

Juhudi mbali mbali anazichukua ikiwemo kukaa chini na viongozi wenzake ikiwemo mbunge na Mwakilishi kwa lengo la kutafuta njia mbadala ya kulitatua tatizo hilo.

“Naelewa kuna athari mbali mbali zinazojitokeza hasa kwa wanawake ikiwemo kupata udhalilishaji kwa kujisaidia nje”, alisema.

Alisema mwaka jana maradhi ya mripuko yalikuwa hamna lakini hawatarajii kutokea kubwa wanachopata wao ni UTI ambayo inatokana na kujisaidia ovyo.

Mwenyekiti mazingira na afya Hamad Ali Maalim alisema kipindi cha nyuma wananchi wengi walikuwa hawana uelewa wa kuchimba vyoo, jambo ambalo lilikuwa linasababisha uharibifu wa mazingira.

Alisema kwa kushirikiana na viongozi walitoa elimu juu ya madhara ya kutokuwa na choo na hatimae baadhi yao wamechimba vyoo, na bado wanaendelea kuwahamasisha.

Aliongeza kuiomba serikali kuwasaidia wananchi wake kwa kuwatafutia wafadhili kwa lengo la kuwachimbia vyoo ili kuepuka kutupa vinyesi ovyo.

Alisema wameweka mkakati kwa wananchi hao kuwa na utaratibu wa kusafisha fukwe kwa sababu ya kusambaa ovyo kwa vinyesi.

Akitoa ufafanuzi juu ya kadhia hiyo Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Ayoub Mohamed Mahmoud alisema umefika wakati wa kufanya tathmini kujua nyumba zilizokosa huduma hiyo kwenye kijiji hicho ili kujua ukumbwa wa tatizo na kutafuta mbinu mbadala za kuwasaida ili kuondokana na hali hiyo kijijini hapo.

“Tunao uwezo wa kuwasaidia mtu mmoja au wawili lakini lazima tuwe na tathmini ya kujua ukubwa wa tatizo kwa lengo la kulipatia ufumbuzi”, alisema.

Ayoub aliwataka wananchi kuwa na subra kwa sababu serikali inaendelea kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo.

Katika kuhakikisha lengo linafikiwa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA Zanzibar) kimekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha wanawake wanawajengea uwezo wa kuwa viongozi.

Mradi huo wa miaka minne uliofadhiliwa na shirika la UN Women unawashirikisha waandishi wa habari wachanga ambao wataibua changamoto za wanawake hao.