MATUKIO ya kibaguzi simageni tena duniani hivi sasa, kwani mataifa tofauti yanakabiliwa na changamoto hiyo ya ubaguzi katika nyanja mbalimbali, haijalishi ubaguzi wa rangi, jinsia, kabila au vyenginevyo lakini bado tatizo litakuwa ndio lilelile tu ubaguzi.

Kutokana na ukubwa wa tatizo hilo hupelekea mivutano katika jamii hadi kuzuka maandamano makubwa na kuathiri watu wengi pamoja na mali zao, kwamfano nchi kama Marekani Afrika Kusini, Ufarasa na kadhalika tayari yaliwa kuzuka maandamano si mara moja na kupelekea uharibufu mkubwa wa miundombinu na hata watu kupoteza maisha.

Aidha licha ya mataifa makubwa kuandaa mipango ya kupunguza wimbo la Ubaguzi ili kuiweka jamii katika hali ya usawa na mshikamano laini bado tatizo la kibaguzi halijaondoka na linaendelea kuitesa dunia kiujumla.

Ndani ya wiki hii, Umoja wa Mataifa umetangaza wazi kuwa, licha ya kupita miongo miwili tangu kupasishwa azimio la Durban lakini bado vitendo vya ubaguzi wa rangi vinaendelea kushuhudiwa katika maeneo mbalimbali ulimwenguni.

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameleza katika hotuba yake kwenye mjadala wa wazi wa ngazi za juu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambao umejikita katika maadhimisho ya miaka 20 ya azimio la Durban na kubainisha kwamba, Miongo miwili baada ya kupasishwa azimio la Durban ambapo lengo lake kuu lilikuwa ni kutokomeza ubaguzi wa rangi na ubaguzi wa aina zingine, jinamizi wa ubaguzi bado ameiandama dunia.

Guterres amesema kuwa, mwanzoni mwa karne hii, viongozi wa ulimwengu na watetezi wa haki za binadamu walisafiri kwenda Durban wakidhamiria kukomesha chuki na ubaguzi ambao uliharibu karne zilizopita.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amebainisha kwamba, maadhimisho ya miaka 20 ya Azimio la Durban na mpango wa utekelezaji yanatoa fursa muhimu ya kutafakari ni wapi tupo na wapi tunahitaji kwenda.

“Ubaguzi wa rangi na ubaguzi wa aina nyingine bado unaenea katika taasisi, miundo ya kijamii, na maisha ya kila siku katika kila jamii. Ubaguzi wa kimuundo na udhalimu wa kimfumo bado unawanyima watu haki zao za kimsingi zakibinadamu.

Waafrika na watu wa asili ya Kiafrika, jamii za wachache, watu wa asili, wahamiaji, wakimbizi, watu waliokimbia makazi, na wengine wengi wote wanaendelea kukabiliwa na chuki, vitendo vya kunyanyapaa, kutengwa, ubaguzi, na vurugu”, alisema Gutierrez.

Hii inaonesha wazi kuwa changamoto za kiubaguzi zimekuwa zikikosesha amani ya ulimwengu na kupelekea athari kubwa kwa vizazi vinavyokuja hapo mbele.

Lakini ikiwa UN wapo katika juhudi za kukabiliana na tatizo hilo baadhi ya mataifa yanaonekana kutotoa ushirikiano wa kutosha katika kujadili njia muafaka ya kuweza kukabiliana na athari za ubaguzi.

Katika kikao cha hivi karibuni cha Umoja wa Mataifa imeripotiwa kuwa baadhi ya mataifa yameususia mkutano wa UN wa kupinga ubaguzi wa rangi yakitajwa baadhi ya mataifa hayo yakiwemo Israel na Marekani.

Hata hivyo, mkutano huo uliofanyika siku ya Jumatano umetoa ahadi ya kuongeza juhudi maradufu ili waweze kukabiliana na vitendo vya ubaguzi wa rangi duniani kwa zingatio la maazimio ya kongamano ya kupinga ubaguzi wa rangi la 2001 la Afrika Kusini.

Kwa kuufanyia marejeo mkutano huo wa Durban, uliofanyika Afrika Kusini takribani ya miongo miwili iliyopita, kulipitishwa azimio ambalo lilionesha kiwango fulani cha kupigwa hatua katika vita dhidi ya ubaguzi wa rangi, ingawa bado kunatajwa ongezeko la vitendo hivyo na kutokuwepo kwa hali ya kuvumiliana kunakowakabili watu wenye asili ya Afrika na makundi mengine.

Pia kulitolewa mfano katika kambi za wakimbizi, kwa makundi tofauti ya watu wakiwemo vijana, wazee, wenye ulemavu hadi wasio na makazi, ikiwa badu lengo kuu ni kutaka kukomesha matukio ya kibaguzi ulimwenguni kote.

Miongoni mwa juhudi mbalimbali zinazohitaji kuchukuliwa ili kuondosha suala la ubaguzi ni kule kupewa kipao mbele kwa masuala ya fidi na haki kwa wenye kubaguliwa.

Inaelezwa kuwa katika mkutano huu wa sasa wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa pamoja na mambo kadha wa kadha, hivyo kumezingatiwa masuala ya fidia na haki kwa wenye kubaguliwa, zingatio likiwa athari za utumwa, ukoloni na mauwaji ya halaiki, na kuwataka watu wenye asili ya Afrika kutafuta stahili zao kwa kutumia taasisi za kimataifa.

Akichangia kwa njia ya video, Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa alieleza kuwa mamilioni ya wenye asili ya Afrika ambao waliuzwa utumwani wamesalia katika mkwamo, wanaishi pasipo maendeleo, kukosa fursa, kubaguliwa na umasikini.

Kutokana na hayo, kiongozi huyo wa Afrika Kusini amelitaka Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuchukua hatua dhidi ya yale maovu yote yalitokea katika kipindi hicho alichokiita kama nyakati za giza.

Aidha kwa upande wa rais Tshisekedi wa DRC ameeleza kuwa hatua ya kutolewa fidia huenda ikatibu majeraha kwa waathirika.

Kadhalika Rais huyo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Felix Tshisekedi amesema ulipaji wa fidia si kwamba utabainisha makosa yaliofanyika wakati huo lakini pia kutibu majeraha ubaguzi na ukandamizaji, vilivyojengwa katika misingi ya utumwa, ubaguzi wa rangi pamoja na ukoloni.

Hata hivyo azimio la baraza hilo pia lilizingatia maovu yanayosababishwa na chuki za kidini ikiwemo wale wanauupinga Uislamu, chuki dhidi ya wageni na upendeleo dhidi ya Wakristo na kadhalika.

Lakini jambo la kushangaza ni pale Israel, Marekani na mataifa mengine yalionekana kususia mkutano huo kwa sababu uliendelea na ajenda ya malalamiko ya mkutano wa Durban wa miaka 20 iliyopita.

Baadhi ya wachambuzi waneleza kuwa Marekani na Israel walijiondoa kwa sababu kuliandaliwa tamko ambalo lilikuwa likilaani vitendo wanavyofanya Israel dhidi ya Wapalestina.

Aidha kwa upande wa nchi ya Jamaica, ambayo ilishiriki katika mkutano huo wa Jumatano ilisema hakukuwa na miito ya kutosha ya kulipa fidia iliyotokana na madhara ya utumwa katika ulimwengu wa siasa za sasa.

Mkutano huo, unaokwenda samba na mkutano wa kila mwaka wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa viongozi wa ulimwengu walisema ubaguzi wa rangi uliwekwa wazi zaidi katika kipindi cha janga la virusi vya corona, na kitendo cha mauwaji ya 2020 ya Mmarekani mweusi, George Floyd, ambayo yalifuatiwa na maandamano makubwa nchini Marekani pamoja na nchi za ulaya na kumepelekea kuzidisha harakati za kupinga vitendo hivyo katika kila pembe ya ulimwengu.