JUBA, SUDAN KUSINI

OFISI ya Umoja wa mataifa ya kuratibu misaada ya Kibinadamu (OCHA) imesema watu zaidi ya 380,000 wameathiriwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zilizonyesha nchini Sudan Kusini.

Taarifa iliyotolewa na OCHA ilisema, asilimia 75 ya watu walioathiriwa na mafuriko hayo ambayo yamepelekea mito kuvunja kingo zake, ni wakaazi wa majimbo mawili ya Unity na Jonglei.

OCHA ilieleza kuwa, barabara za majimbo yaliyoathiriwa na mafuriko hayo hazipitiki, huku ikionya kuwa, mvua na mafuriko zaidi yanatarajiwa kushuhudiwa nchini humo katika miezi ijayo.

Hadi sasa hakujatolewa idadi ya watu waliofariki dunia na hasara iliyosababishwa na mafuriko hayo katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.

Mvua kubwa zilizonyesha mwaka jana zilivunja rikodi nchini Sudan Kusini, huku mafuriko na maporomoko ya udongo yakiwaathiri watu zaidi ya 700,000.

Katika nchi jirani pia, mafuriko makubwa yaliyosabishwa na mvua kubwa iliyonyesha nchini Sudan yameathiri na kubomoa maelfu ya nyumba za raia hususan huko Khartoum mji mkuu wa nchi hiyo.