SIMU ya mkononi ni kifaa kidogo chenye athari kubwa kwa maisha yetu na kwa wanaokitumia vizuri kuna manufaa makubwa.

Ulimwengu wa teknolojia unamaanisha kwamba matumizi ya simu ya mkononi ni jambo la kawaida, ambapo kila mwaka mamilioni ya watu wanaingia katika kundi la wanaoanza kutumia simu za mkononi.

Hata hivyo matumizi ya simu za mkononi ambayo mwanzoni watu wengi hawakuwa wakijua yanaweza kuvuruga maisha yao sio tu kiafya bali pia kisaikolojia na hata kuhatarisha maisha yao.

Iwapo ulikuwa hutambui kwamba simu yako ya mkononi unayotumia kila siku inaweza kuyavuruga maisha yako, haya hapa ni baadhi ya madhara unayoweza kuyapata kutokana na matumizi ya simu yako endapo hutakuwa muangalifu.

Simu inaweza kubadilisha tabia yako kijamii: Kuna ushahidi wa wazi ambao wanasaikolojia wanasema matumizi ya simu yanaweza kubadilisha tabia ya mtu hasa kijamii.

Sio jambo la ajabu kujua kwamba kwa sasa kuna watu hasa vijana ambao matumizi ya simu yameathiri sana uwezo wao hata kutangamana kwa njia ya kawaida.

Wamezoea kutumia simu na wakati wasipokuwa na simu zao mkononi maisha kwao yanakuwa sio ya kawaida na hata wanaweza kujihisi wagonjwa. Mara ngapi unazungumza na mtu lakini hata hakuangalii?

Hilo hutokana na mazoea ambayo iwapo hayaangaliwi yanaweza kuwa uraibu unaovuruga kabisa jinsi mtu anavyotangamana na wengine kijamii. Je, umewahi kuiweka kando simu yako kwa muda wa saa 24?

Ulihisi ni kama kuna kitu unachokosa maishani mwako? Basi kuna watu wasioweza kuendelea na shughuli zao kamwe bila kuwa na simu zao mikononi.

Kutumia simu ukiendesha gari au ukifanya kazi inayohitaji umakinifu: Umesikia kuhusu ajali za barabarani zinazosababishwa na madereva ambao wanaendesha gari wakitumia simu za mkononi.

Kuna takwimu nyingi kuhusu idadi ya maafa yanayosababishwa na ajali kama hizo na kumekuwa na kampeni kote duniani na hasa kutoka kwa polisi kuhusu hatari ya kuendesha gari ukitumia simu.

Visa pia vipo kuhusu watu ambao wanafanya kazi zinazoweza kutajwa kama hatari ambao wanajitia hatarini hata zaidi kwa kutumia simu. Iwapo utajikuta katika hali kama hizo, unashauriwa kuiweka pembeni simu yako mpaka ufike hatua unayoweza kuitumia.

Umetumiwa pesa kwenye simu ukazitoa na sio zako? Umeyaskia hayo kuhusu watu kuzitumia simu vibaya kwa kutoa fedha wanazotumiwa kimakosa.

Kwa muda mrefu watu wamekuwa wakitumia simu kama kinga ya kufanya maovu na uhalifu. Sheria zinabadilika na kuboreshwa na usije ukadanganyika kwamba unaweza kutekeleza uhalifu kutumia simu yako ukifikiri uko salama.

Hakikisha unanunua simu kwa njia halali ama kwa muuzaji mwenye leseni: Iwapo ulifikiri unaweza kuinunua simu ya mkononi kwa yeyote kwa sababu umeipata kwa gharama ya chini, itabidi ufikirie tena uamuzi huo.

Kuna hatari kubwa sana kununua simu kutoka kwa mtu yeyote. Kunayo mifano ya watu waliofungwa jela kwa makosa makubwa hata ya mauaji kwa kuuziwa simu ambazo zilipatikana kupitia uhalifu.

Amekuuzia mtu simu kwa gharama ya chini kumbe ni simu ya wizi ambayo hata ilisababisha mwenyewe kuuawa.

Wakati polisi inapofanya uchunguzi na kuifuata simu hiyo, unakutikana nayo wewe bila kujua ilikotoka na visa ni vingi vya watu wanaopambana na kesi mahakamani kuhusu kununua vifaa vya elektroniki kwa njia kama hiyo.

Hakikisha simu unayonunua ni halali kutoka kwa muuzaji unayeweza kuthibitisha kwamba alikuuzia simu hiyo.