NA MWAJUMA JUMA

UMOJA wa Mataifa kupitia mpango wa kujitolea ‘United Nation Volunteers’ (UNV), wamo katika mchakato wa kutafuta vijana wa kizanzibari wenye sifa na vigezo vitakavyowawezesha kuingia katika programu za kujitolea ndani na nje ya Zanzibar.

Mpango huo unafanyika kwa mashirikiano ya karibu na mpango wa kujitolea Tanzania hivyo kupitia mpango huo unawatangazia vijana hao wenye utaalamu wa kada tofauti kutumia fursa ili waweze kushiriki katika mpango huo.

Shirikia hilo limekuwa likipita katika vyuo mbali mbali kutoa elimu kwa wanafunzi ambao wanakaribia kuhitimu masomo yao.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mtaalamu wa dimbwi la vipaji wa umoja huo Penina Nguma alisema, wanafanya hivyo kwa sababu katika vyuo kunakuwa na vijana wengi wenye utaalamu ambao wataweza kukidhi vigezo ambavyo vinatakiwa.

Nae mwakilishi mkaazi wa umoja huo Christian Mwamanga, alisema kwamba mchakato huo unatafuta vijana wa kada tofauti wenye umri kuanzia miaka 18 hadi 35.

Alizitaja kada hizo ni mtaalamu bingwa wa mataifa wa kujitolea, mtalamu wa Umoja wa Mataifa kujitolea, kijana wa umoja wa mataifa wa kujitolea na kijana wa umoja wa mataifa kwa njia ya mtandao.

“Huu ni mpango unaotoa fursa sawa kwa kukaribisha maombi kutoka kwa wataalamu wenye sifa, tumejitolea kufika utofauti katika suala la jinsia, utaifa na utamaduni”, alisema.

Alisema kwa wale ambao watapata fursa hizo wahakikishe wanafungua akaunti mtandaoni na kuingiza taarifa zote na kuwa wazi wakati wowote ili kupata mawasiliano muda wote.