CONAKRY, GUINEA

WANASIASA wa muda mrefu wa upinzani nchini Guinea wametoa matamshi ya kuwaunga mkono watawala wapya wa kijeshi katika siku ya kwanza ya mkutano wa siku nne ulioitishwa kujadili hatma ya taifa hilo baada ya mapinduzi ya mwanzoni mwa mwezi Septemba.

Viongozi wa vyama vya upinzani nchini humo walielezea kuridhishwa na uamuzi wa kumpindua rais Alpha Konde ambaye mwaka jana alirejea madarakani kwa muhula wa tatu baada ya kufanya mabadiliko ya katiba yaliyozusha wimbi kubwa la maandamano.

Kiongozi wa chama cha upinzani cha PDP Ousmane Kaba alisema uamuzi wa Konde wa kurefusha utawala wake ulikuwa kinyume na sheria na mapinduzi yaliyotokea yanalenga kuirejesha Guinea kwenye mkondo wa utawala wa katiba.

Mwanasiasa mashuhuri wa upinzani nchini Guinea Cellou Diallo, alimtaja Konde kuwa kiongozi dikteta aliyejitengezea njia ya anguko lake mwenyewe.

Watawala wa kijeshi walianzisha mashauriano ya kitaifa katika wakati shinikizo linaongezeka la kuwataka kuitisha uchaguzi wa kidemokrasia na kuirejesha Guinea kwenye utawala wa kiraia.