NA MWANDISHI WETU

NI ukweli usiofichika kwamba uchafu wa mazingira, pamoja na tabia ya uchafu waliyonayo baadhi ya wananchi, inachangia sana kuenea kwa maradhi mbalimbali yanayoua haraka ikiwemo kipinduindu.

Kwa hivyo, hatuna budi sote kwa pamoja kuzingatia na kufuata malekezo ya wataalamu pamoja na kanuni za afya kwa kuimarisha usafi, ili tuepukane na maradhi.

Hakuna asiyejua kwamba usafi ni jambo muhimu kwa binadamu, na hata vitabu vya dini vinahimiza waumini kuwa wasafi wa tabia na vitendo katika sehemu wanazoishi.

Kwa muktadha huo, nachukua fursa hii kuwatanabahisha wananchi wote, kwanza kuwa wasafi wao wenyewe na pia kujiwekea na kuuendeleza utamaduni wa kusafisha mazingira.

Katika hili, tuache kusubiri kutokea kwa majanga, mathalan maradhi ya mripuko kama vile homa za matumbo zinazoenena kwa haraka sana na kuathiri jamii.

Usafi wa nyumba zetu tunazoishi, maofisi na maeneo mengine tunayofanyia kazi hasa sehemu za biashara ya vyakula na vinywaji, liwe jambo la lazima na tuliwekee kanuni kwa yeyote atakayepuuza.

Uzoefu unaonesha kuwa, sehemu zetu tunazofanyia biashara za vyakula na vinywaji, haziwekwi katika mazingira safi, hali inayochangia mripuko wa maradhi ambayo hatimaye huishia kupukutisha roho za watu wengi.

Kwa hivyo, tutumie uzoefu wa visiwa vyetu kukumbwa na maradhi ya kipindupindu kubalisha hulka zetu na kuwa watu wanaouchukia uchafu badala ya kuukumbatia.

Ni wajibu wetu sote kuchimba karo za kupitishia maji machafu, kutunza vyema sehemu za biashara na pia kuhifadhi vyombo vinavyotumika kwa kupikia mikahawani na majumbani mwetu.

Aidha ni jukumu la wazazi na walezi kuwalinda watoto wetu na kuwaelimisha juu ya kutunza  usafi hasa wakati huu mvua zikiendelea kunyesha hapa visiwani kwetu.

Kamwe tusiache kula bila kwanza kunawa mikono tena kwa maji ya mtiririko na sabuni na pia kufanya hivyo baada ya kwenda haja, halikadhalika tuwakataze watoto wetu tabia ya kula ovyo wanapokuwa mbali nasi.

Lazima tuelewe kwamba janga la kipindupindu linapoingia sio la mtu au kikundi cha watu maalumu, bali ni letu sote kwa sababu kila mmoja kuna uwezekano kukipata.

Hivyo kila mmoja katika nafasi yake, anapaswa kuchukua tahadhari, hasa tukizingatia kuwa linaweza kumpata yeyote, awe mtoto au mtu mzima.

Miongoni mwa mambo ya msingi tunayohimizwa na wataalamu wetu, ni kutumia maji yaliyochemshwa au kuwekwa dawa ya kutaibu yaani ‘Water Guard’ kwa kunywa.

Lakini hili tusiwe tunalifanya wakati nchi ikiwa na maradhi ya mripuko tu, bali iwe tabia yetu ya kila siku, tukizingatia usemi wa ‘Kinga ni bora kuliko tiba.’

Kwa upande mwengine, ninapenda kuwashauri watu wanaofanya biashara ya mikate katika masusu mitaani, kuhakikisha wanunuzi hawachagui kwa kushikashika kila mkate, kwani hatuwezi kujua walikotokea na wameshika kitu gani kabla.

Nanyi pia mnapaswa kuweka vibanio au hata karatasi zilizo safi kwa ajili ya kushikia mikate na kuweka kwenye mikoba ya wateja wanu.

Pamoja na wananchi kutakiwa kuzingatia usafi, Baraza la Manispaa pamoja na Halmashauri zetu nazo zijitahidi kuchukua taka kwenye makontena kwa wakati, ili kuepuka kuzalisha nzi kwa wingi kutokana na uvundo unaosababishwa na taka zilizorundikana muda mrefu na kuroa kwa mvua.

Ili kurahisisha manispaa kuondoa taka kwa wepesi, ni busara nasi wana jamii kuhakikisha tunazitia taka hizo kwenye makontena yaliyowekwa mitaani kwa ajili hiyo badala ya kuzimwaga ovyo ardhini.

Tujitahidi kutumia kanuni zote tunazopewa na Wizara ya Afya kwa kutupa elimu kwenye matumizi yetu ya kila siku tusiidharau elimu hii kwa kuzingatia usafi kwani elimu hii ni mfano tosha tulivyoweza kuifuata na dalili sasa.