TUPONGEZE serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa uamuzi wake wa kufungua milango na hatimaye kuikaribisha sekta binafasi kuwekeza kwenye miradi mbalimbali hapa nchini.

Kuruhusiwa kwa uwekezaji hapa nchini msingi wake umelenga kuimarisha, kurahisisha na kuwezesha kupatikana kwa huduma muhimu na za msingi kwa wananchi.

Kutokana na hatua hiyo, wawekezaji wa kigeni na wenyeji wameitumia vyema fursa ya uwekezaji kwa kuwekeza kwenye miradi ya aina mbalimbali ikiwemo ya utoaji wa huduma za jamii.

Kwa mfano wapo wawakezaji wazalendo wamewekeza kwenye sekta ya afya kwa kujenga kliniki, vituo vya afya pamoja na maduka ya uuzaji wa dawa za kutibu maradhi mbalimbali.

Wengine wamewekeza kwenye sekta ya elimu ambapo wamejenga skuli kuanzia za chekechea hadi sekondari wakiwapatia elimu inayolingana na mtaala wa taifa watoto katika jamii yetu.

Kwa hakika uwekezaji kwenye sekta ya elimu una umuhimu wa aina yake kwa hapa Zanzibar kwani umewapa fursa wananchi kuchagua kuwapeleka watoto wao kwenye skuli za serikali ama zile zinazomilikiwa na watu binafsi.

Uwekezaji kwenye skuli binafsi umepunguza mzigo kwa serikali katika kuwapatia huduma za elimu watoto wa hapa Zanzibar hasa ikizingatiwa kuwa inabeba gharama kubwa kutoa elimu bila malipo.

Hata hivyo, kwa muktadha wa tahariri hii tungependa kujikita zaidi kuzielezea changamoto zilizopo kwenye sekta ya uwekezaji binafsi kwenye sekta ya elimu.

Kweli wawekezaji wametumia fursa ya kujenga skuli na kutusomeshea watoto wetu, lakini lazima changamoto zilizopo zirekebishwe kabla ya kujitokeza kwa athari kubwa.

Kwanza kabisa tungependa kuieleza wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali hapa Zanzibar, lazima ihakikishe inasimamia suala la skuli binafsi zinafuata mitaala iliyopitishwa na kukubaliwa na serikalini.

Hili limekuwa tatizo kubwa kwani zipo baadhi ya skuli binafsi kwa mtazamo wa nje zinajifanya zinatumia mitaala ya hapa nchini, lakini ukaweli ni kwamba kichini chini wanafuata mitaala kutoka nje ya nchi.

Suala hilo lazima lifanyiwe uchunguzi wa kina na pengine ndio sababu inayochangia wanafunzi wengi kushindwa kufanya vizuri katika mitihani yao ya taifa.

Wazee wengi hupeleka wanafunzi kwenye skuli binafsi wakati mwengin kutokana na kutokuwa na muda, hivyo mbalimbali ya kuwalipia huduma za masomo pia hulipa gharama za usafiri.

Kwa bahati mbaya sana baadhi ya mabasi ya skuli binafsi yanayopakia wanafunzi na huwajaza watoto hao kama makumbi jambo linakiuka sheria za usalama barabarani.

Tunawaeleza madereva wa mabasi ya skuli binafsi kwamba kuwapakia wanafunzi hakutoi fursa ya namna yoyote kukiukwa sheria za usalama barabarani kwa njia yoyote ile.

Tunalitaharisha hili sio kama tunaomba lakutokea hapana, lengo letu ni kutaka sheria za usalama barabarani zifuatwe kikamilifu ili kuepuka madhara ambayo yanaweza kuiachilia kilio jamii yetu.

Tungeomba sana polisi kitengo cha usalama barabarani walishughulikie hili, lakini pia wazifanyie ukaguzi wa mara kwa mara gari hizo.

Lengo letu sio kuingilia kwa kuharibu biashara za watu, bali tunachotaka ni kuhakikisha ajali zinaoweza kuzuiliwa wenye dhama hiyo wanatekeleza.