LONDON, UINGEREZA

KATIBU Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amesema kwamba anakhofia kurejea madarakani kwa kundi la Taliban nchini Afghanistan kutayachochea makundi mengine ya siasa kali katika ukanda wa Sahel.

Akizungumza na shirika la habari la AFP, Guterres alisema kuna hatari ya makundi hayo kutiwa moyo na kilichotokea Afghanistan na kurejea kwenye uwanja wa mapigano kwa malengo ya kufikia walipofikia Taliban.

Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa alitowa wito wa kuimarishwa kwa mifumo ya usalama katika ukanda wa Sahel, akisema kwamba sasa makundi hayo yalisambaa kutoka Mali, Burkina Faso, hadi Ivory Coast na Ghana.

Kauli ya Guterres inakuja wakati Ufaransa ikiazimia kupunguza wanajeshi wake kwenye ukanda huo, huku Chad ikiondosha kabisa wanajeshi wake katika mpaka wa Burkina Faso, Niger na Mali.