NA KHAMISUU ABDALLAH

IMEELEZWA kuwa Tanzania ni moja ya nchi iliyokua kidemokrasia kuliko nchi nyengine zilizopo Afrika Mashariki kutokana na kuwepo kwa uhuru, usawa na ushirikishwaji wananchi kutoa maamuzi kwa mujibu wa katiba.

Mrajis wa Jumuiya zisizo za kiserikali (NGO) Zanzibar, Ahmed Abdulla, alieleza hayo wakati akifungua mdahalo uliolenga kubadilishana mawazo ili kuimarisha maarifa, taaluma, ujuzi na weledi kuhusu wajibu wa wadau wa kisiasa katika kujenga na kusimamia utekelezaji wa misingi ya mfumo wa demokrasia ya vyama vingi nchini Tanzania.

Katika mdahalo huo unaofanyika kwa siku tatu katika hoteli ya Abla Sharifumsa, Ahmed alisema Tanzania imepiga hatua kubwa ya demokrasia kwani ni nchi yenye amani, umoja na mshikamano na watu kuwa na uhuru wa kufanya shughuli zao kwa kufuata sheria za nchi ambayo ndio demokrasia.

“Tumeona jinsi viongozi wa serikali kuu wanavyoshuka kwa wananchi kusikiliza kero zao na kupata mashauriano lakini pia Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameanzisha mfumo wa Sema na Rais Mwinyi ambao umedhamiria kuwafikia wananchi,” alisema.

Akizungummzia lengo la mdahalo huo, alisema una umuhimu mkubwa katika kutathmini mwenendo wa nchi katika hatua za maendeleo na serikali inavyojitahidi katika kukuza demokrasia nchini.

Ahmed aliipongeza Taasisi ya Mwalimu Nyerere Tanzania kwa kuamua kufanya mdahalo huo ambao unawapa hamasa ya uwajibikaji katika kutekeleza shughuli zao mbali mbali za maendeleo.

Aliwaomba wananchi kuendeleza umoja, amani na mshikamano uliopo nchini ili nchi yao iendelee kupiga hatua za kimaendeleo kwani Amani, umoja na mshikamano ndio chachu kubwa ya kuendeleza demokrasia nchini Tanzania.

Mbali na hayo, alisema ni imani yake kwamba washiriki wa mdahalo huo watatumia nafasi hiyo itakayoweza kuleta matukio chanya ambayo yatakayoendeleza umoja, mshikamano, demokrasia na mambo mengine.

Mapema Mkurugenzi Mtendaji na Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini wa taasisi hiyo, Joseph Butiku, alisema mdahalo huo una lengo la kuendeleza mazungumzo yanayohusu mfumo wa kidemokrasia uliopo nchini.