NA ALI ISSA, MAELEZO

SERIKALI ya Oman imesema kuwa itaipatia Zanzibar kifaa maalum cha kuangalia muandamo wa mwezi, ambacho kinatarajiwa kuwasili nchini kabla ya kufikia mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Balozi mdogo wa Oman, aliyepo Zanzibar Said Salum Al-Sinawi alieleza hayo jana wakati alipofanya mazungumzo na Mufti wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kaabi.

Balozi huyo pia alitumia fursa hiyo kujitambulisha kwa Mufti wa Zanzibar baada ya kuteuliwa na nchi yake kuja kuiwakilisha hapa Zanzibar kufuatia aliyekuwa kwenye nafasi hiyo kumaliza rasmi muda wake wa kuhudumu hapa nchini.

Balozi Al-Sinawi alisema wananchi wa Zanzibar na waoman ni watu wenye udugu wa damu kwa muda mrefu, hivyo ipo haja nchi hiyo kusaidia katika maeneo ambayo yatakuza maendeleo ya wananchi.

“Mimi naelewa kuwa Zanzibar na Oman tuna udugu wa damu, niwahakikishie kuwa tutakuwa pamoja ili kukuza na kuendeleza udugu wetu”, alisema balozi huyo.

Alifahamisha kuwa anachokifanya hivi sasa ni kuangalia maombi yote ya miradi mbalimbali yaliyofika ofisini kwake na yale ambayo yamepangwa kutekelezwa na kwamba kazi yake ni kuongeza nguvu kwa kuhakikisha miradi yote inatekelezwa.

“Nimeona maombi yenu mara tu baada ya kufika ofisini ni jambo jema nitashughulikia hilo ni masuala muhimu kuweza kutekeleza”, aliongeza kusema balozi huyo.

Alieleza kuwa maombi yao yapo mezani ikiwemo maombi ya uendelezaji wa ujenzi wa Ofisi ya Mufti, kifaa cha kuangalizia mwezi na mambo mengine mengi ambayo ni muhimu kwa maendeleo na ustawi wa wananchi wa Zanzibar.

Kwa upande wake, Mufti wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kaabi, alimshukuru kiongozi huyo kwa ujio wake kufika ofisini hapo na kusema ujio huo ni kuendeleza udugu wao wa damu ambao Zanzibar inafaidika sana na misaada kutoka serikali ya Oman ikiwemo ujenzi wa misikiti, nyumba za kihistoria, vyuo na maeneo mengine ya kijamii.