NA MADINA ISSA

UMOJA wa Wanawake Tanzania (UWT) wa Chama cha Mapinduzi (CCM), umesema unamuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa kauli yake ya kuwaomba wanawake kuhakikisha wanamuweka madarakani Rais mwanamke ifikapo mwaka 2025.

Makamu Mwenyekiti wa umoja huo Taifa, Thuwaiba Edington Kisasi aliyasema hayo, alipokuwa akitoa tamko hilo mbele ya makatibu wa mikoa na wilaya za jumuiya hizo katika Afisi Kuu Kisiwandui.

Kisasi alieleza kuwa UWT Zanzibar inaunga mkono hotuba iliyotolewa na Rais Samia aliyoitoa Septemba 15 mwaka huu, waliyosema imeongeza hamasa ya wanawake kuwania nafasi za uongozi ndani nan je ya chama.

“Tunamuunga mkono Rais Samia pamoja na jitihada zake anazoendelea kuzionyesha kwa vitendo wanawake katika kuwapa nafasi mbali mbali za uongozi na kuendelea kuleta mabadiliko chanya ya nchi yetu ya Tanzania,” alisema.

Alisema UWT ina mpongeza Rais Samia kwa kusimamia utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2025 kwa vitendo na kwamba fursa hiyo jumuiya hiyo imeona namna anavyopambana kwa kutoa nafasi nyeti kwa wanawake.

“Tunamuhaidi kumpa ushirikiano ya dhati katika kuwatumikia wa Tanzania sisi wanawake tunakuhakikishia tutafanya kazi kwa bidii katika kusimamia na kutekeleza ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025 hivyo tunahaidi kuongeza mshikamano na upendo ili ifikapo mwaka 2025 tunamuweka Rais mwanamke madarakani,” alisema

Makamu huyo Mwenyekiti alisema UWT Zanzibar ina muhaidi Rais Samia kuendelea kulinda Muungano wa serikali mbili ikiwemo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na kuyalinda,kuyatetea na kuyasemea mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya Januari 12 mwaka 1964.