LONDON, England
LIVERPOOL imelazimika kutoka nyuma kushinda magoli 3-2 dhidi ya AC Milan kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyochezwa uwanja wa Anfield.
Kikosi cha Jurgen Klopp kililizingira lango la Milan tangu mwanzo wa mchezo, wakichukua uongozi uliostahili mapema wakati beki wa zamani wa Chelsea, Fikayo Tomori alipopangua krosi kutoka kwa Trent Alexander-Arnold na kwenda kwenye nyavu zake mwenyewe.
Liverpool ambayo ilikosa nafasi ya kuzidisha magoli wakati penalti ya Mohamed Salah ilipookolewa na kipa, Mike Maignan, walishangazwa na Milan baada ya kufunga mara mbili katika dakika mbili na kuchukua uongozi kupitia, Ante Rebic na Brahim Diaz.
Lakini, magoli ya Salah kwenye dakika ya 48 na Jordan Henderson yakawapaisha mabingwa hao wa zamani wa Ulaya.
Nchini Ubelgiji, licha ya kuongozwa na nyota watatu wakubwa duniani, Lionel Messi, Kylian Mbappe na Neymar, Paris Saint-Germain iliambulia sare ya 1-1 dhidi na wenyeji, Club Bruges.
Mchezo huo wa kundi ‘A’ ulipigwa uwanja wa Jan Breydel jijini Brugge, Ubelgiji.
PSG ilitangulia kwa goli la kiungo Mspaniola, Ander Herrera, kunako dakika ya 15 kabla ya kiungo Mbelgiji, Hans Vanaken kuisawazishia Club Bruges mnamo dakika ya 27.
Mabingwa England, Manchester City wameibuka na ushindi wa magoli 6-3 dhidi ya RB Leipzig katika mechi iliyochezwa uwanja wa Etihad.
Magoli ya ManCity yalifungwa na Nathan Ake (dk.ya 16), Nordi Mukiele aliyejifunga (dk.ya 28), Riyad Mahrez (dk.ya 45), Jack Grealish (dk. ya 56), Joao Cancelo (dk.ya 75) na Gabriel Jesus (dk. ya 85), wakati ya RB Leipzig yote yalifungwa na Christoph Nkunkukwenye dakika ya 42, 51 na 73.
Beki wa zamani wa ManCity, Angelino alitolewa kwa kadi nyekundu 79 kufuatia kuonyeshwa kadi ya pili ya njano.Nchini Italia, wenyeji Inter Milan walilala goli 1-0 nyumbani mbele ya Real Madrid huku goli pekee likifungwa na yoso wa Brazil mwenye umri wa 20, Rodrygo Goes kwenye dakika ya 89.
Mechi hiyo ya kundi ‘D’ ilipigwa uwanja wa Giuseppe Meazza jijini Milan.Matokeo mengine ya michuano hiyo, Besiktas 1 vs B. Dortmund 2, Sheriff Tiraspol 2 vs Shakhtar Donetsk 0, Atletico Madrid 0 vs FC Porto 0 na Sporting 1 vs Ajax 5. (Goal).