NA HAFSA GOLO
KATIBU wa chama cha Mapinduzi (CCM) jimbo la Donge, Haji Boko, amewataka vijana kuunga mkono juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na viongozi wao wa jimbo hilo, ili kuimarisha hali za wananchi kiuchumi na kijamii.
Aliyasema hayo wakati akizungumza na vijana na wanachama wa CCM jimboni humo katika kikao cha kutathmini miradi ya maendeleo na utatuzi wa kero za wananchi katika ofisi ya Chama cha Mapinduzi Donge Mbiji.
Alisema viongozi hao wamekuwa mstari wa mbele kushajihisha, kuelimisha pamoja na kuwawezesha wananchi kitaaluma, ili waweze kujiajiri wenyewe kwa kutumia sekta ya kilimo na biashara.
Aidha, alisema utaratibu huo ni mzuri katika kuleta mageuzi ya kiuchumi ndani ya jamii jambo la msingi ni uwajibikaji na kuzingatia uchapakazi.
“ Uchaguzi umeisha hivyo ni jukumu la vijana na wananchi kwa pamoja kushirikiana na viongozi hao katika ujenzi wa miradi ya maendeleo jimboni humo nakufuata maelekezo yao”,alisema.
Alisema ushiriki wao katika masuala ya maendeleo ni jambo muhimu linalihitajika kupewa kipaumbele na kila mtu ili kusaidia kufikia azma ya serikali katika mikakati na mipango ya maendeleo ngazi ya jimbo hadi taifa.
“Vijana nyinyi ni nguvu kazi ya taifa hivyo,nawanasihi kushirikiana na viongozi wenu wa serikali na jimbo katika suala zima la maendeleo sambamba na kuendelea kubuni miradi ya maendeleo ambayo yatakuwa na manufuaa kwetu na kuleta mageuzi ya kiuchumu”,alisema.
Mmoja wa vijana hao aliejitambulisha kwa jina la Mwanaisha Juma, alisema kwamba wanatambua mchango wao vijana ndio nguzo imara ya kuleta mageuzi ya maendeleo n ahata kukipatia ushindi chama hicho.
Hivyo aliahidi kutumia busara na hekma katika ushajihishaji wa jamii katika umuhimu wa mashirikiano katika ujenzi wa miradi ya maendeleo.