NA ASYA HASSAN
MWAKILISHI wa Jimbo la Malindi, Mohamed Ahmada Salum, amewataka vijana wa Jimbo hilo kuandaa miradi mbalimbali ya maendeleo itakayoweza kutoa tija ndani ya jimbo hilo na taifa kwa ujumla.
Ahmada alisema hayo alipokuwa akizungumza na wananchi wa shehia ya Mwembetanga Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, ikiwa ni miongoni mwa ziara zake za kusikiliza kero na changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa Jimbo hilo.
Alisema hatua hiyo itasaidia kwa vijana hao kupata ajira pamoja na kuondosha vikundi viovu na kupunguza uhalifu ndani ya jimbo hilo na maeneo jirani.
Mwakilishi huyo, alifahamisha kwamba tatizo la ajira limekuwa sugu katika nchi mbalimbali duniania hali ambayo serikali imekuwa ikitafuta mbinu tofauti, ili kuona vijana wanapata fursa ya kujiajiri, na kuondokana na tatizo lakusubiri ajira serikalini.
Sambamba na hayo alisema vijana wanawajibu wa kulitumikia taifa lao, ili kuleta maendeleo katika nyanja mbalimbali ikiwamo katika kuongeza pato la ukuwaji wa uchumi na sio kujishirikisha katika mambo yanayoendana kinyume na maadili yao.
Aidha, alitumia fursa hiyo kuwataka vijana hao wasikubali kutumiwa katika mifumo isio rasmi, ambayo itasababisha kuvuruga mfumo mzima wa maisha yao na taifa kwa ujumla.
Nae Sheha wa Shehia ya Mwembetanga, Ramadhani Omar, alisema matatizo yote yanahusiana na masuala ya uhalifu ndani ya shehia hiyo ameshayafikisha sehemu husika, ili kuona vitendo hivyo vinachukuliwa hatua zinazostahiki.