NA MWAJUMA JUMA

MRAJISI wa Vyama Vya Michezo na Klabu Zanzibar  Abubakar Mohammed Lunda,  amewazuia na kuwafungia kwa muda wa miaka mitano, waliokuwa viongozi wa Chama Cha Mpira wa Kikapu Zanzibar (BAZA) kwa utovu wa nidhamu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa inasema viongozi hao wanadaiwa kufanya makosa mawili, moja kutoa taarifa ya uongo dhidi ya kiongozi, ikiwa ni  kinyume na kifungu cha 21(2) (b).

Kosa la pili ambalo walilifanya ni kumkashifu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo kinyume na kifungu cha 21 ( C ), kanuni za usajili wa vyama na klabu za mwaka 2014.

Barua hiyo ambayo ilitolewa Septemba 7 mwaka huu, iliwataka viongozi hao kutii adhabu hiyo, ambayo imetolewa kwa maslahi mapana ya mchezo huo Zanzibar.

Mrajisi kupitia barua hiyo wametakiwa kutojihusisha na shughuli zozote za michezo kuanzia siku iliyotoka barua hiyo.

Waliofungiwa ni Mwenyekiti wa chama hicho Ramadhan Khamis Salmini, Makamu Mwenyekiti Rashid Hamza Khamis na wajumbe Masoud Salim Ali, Mohammed Juma Sharif na Stara Khamis Salum.

Wengine ni Mwache Mohammed Bakar, Bimkubwa Omar Khatib, ambao wote kwa mujibu wa Mrajisi wamepatiwa barua zao.