NEW DELHI, INDIA

VIONGOZI wa kundi la nchi zinazoibukia kiuchumi, BRICS wamesisitiza kwamba Afghanistan haiwezi ikawa maficho ya magaidi.

Wakuu wa nchi za BRICS ambazo ni Brazil, Urusi, India, China na Afrika Kusini wanaamini wana ushawishi mkubwa kwa maswala ya kimaeneo.

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi aliandaa mkutano wa kundi hilo uliofanyika kwa njia ya mtandao.

Walijadili ugaidi, usalama na haki za binadamu, hasa namna ya kulinda wanawake wa Afghanistan, watoto na makabila ya walio wachache.

Rais wa Urusi Vladimir Putin aliwalaumu viongozi wa Marekani kwa hali waliyoiacha nyuma walipoondoa wanajeshi wao wiki iliyopita.

Alisema janga hilo linatokana na kile alichokiita majaribio yasiyo na uwajibikaji ya ulazimishaji wa maadili ya kigeni.

Putin alisema Afghanistan haipaswi kuwa tishio kwa majirani zake au chanzo cha ugaidi na ulanguzi wa dawa za kulevya.