NA KHAMISUU ABDALLAH

VYAMA vya siasa nchini zimeshauriwa kuendelea kudumisha amani ya nchi ili Zanzibar iendelee kupiga hatua kubwa za kimaendeleo.

Meya wa Jiji la Zanzibar, Mahmoud Mohammed Mussa, aliyasema hayo wakati akifungua mdahalo wa kitaifa wa kuimarisha udugu, uzalendo, uwajibikaji amani maridhiano na maendeleo ya nchi ulioshirikisha viongozi wa serikali, vyama vya siasa na asasi za kiraia uliofanyika katika ukumbi wa shirika la Bima Zanzibar, Mpirani.

Alisema jambo hilo ni muhimu na jema kwa mustakabali wa nchi kwani hujenga misingi imara iliyoasisiwa na waasisi wa taifa la Tanzania Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume.

Mahmoud, alibainisha kuwa jambo kubwa wanalojivunia Watanzania ni uwepo wa amani na utulivu wa nchi kwani jambo hilo linasababisha hata nchi zilizokuwepo mataifa ya nje kuipa sifa Tanzania hivyo aliamini kwamba wataendelea kutunza amani ya nchi yao.

Aidha, alisema wananchi watambue kuwa Tanzania na Zanzibar itajengwa na wananchi wenyewe na hakuna mtu atakaetoka nje kufanya jambo hilo kuja kuleta maendeleo ya nchi yao hivyo ni jambo jema kuendelea kufanya vizuri kwa maslahi ya taifa lao.

Hata hivyo, alibainisha kuwa pamoja na Muungano uliopo lakini vyama vya siasa vilipata uhuru wa kufanya mambo yao mwaka 1962 ambapo mpaka leo wanajivunia kwa hilo.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, alisema taasisi yao ina lengo la kushughulikia amani, umoja na maendeleo ya wote na lengo hilo litekelezwe kwa kushirikiana na serikali, wananchi, Bungee, Baraza la Wawakilishi na vyombo vya ulinzi na usalama ndani na nje ya nchi yao.

Alisema Mwalimu Nyerere lengo lake lilikuwa ni kuona nchi inaendelea kuwa na amani kwani hakuna mtu anaependa machafuko na kukosa furaha na ubora wa maisha.

Aidha alizipongeza serikali zote mbili kwa kukubali taasisi ya mwalimu Nyerere kushirikiana na Jumuiya ya Marekani ya Insitute Repaplic Insitute (IRI) kwa lengo la kutoa elimu ya demokrasia, uzalendo maridhiano na amani nchini.