NA MWINYIMVUA NZUKWI
VYOMBO vya habari vimetakiwa kuongeza jitihada za kuwahamasisha wanawake kujiandaa kuwania nafasi za uongozi ili kutimiza azma ya serikali ya kuwa na uwakilishi sawa baina ya wanawake na wanaume kwenye vyombo vya maamuzi.
Wito huo umetolewa na Mtafiti wa maswala ya habari na mawasiliano, Dk. Aboubakar Sheikh Rajab, alipokuwa akiwasilisha matokeo ya utafiti kuhusu habari zinazowahusu wanawake viongozi, katika ofisi za Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA – Zanzibar), Tunguu, wilaya ya Kati Unguja.
Alieleza kuwa katika kipindi cha mwezi novemba na disemba 2020, vyombo vya habari viliripoti kwa uchache habari za viongozi wanawake ikilinganishwa na viongozi wanaume jambo linanoibua hisia za upendeleo.
Alisema ili kurekebisha hali hiyo, vyombo vya habari vinapaswa kuwa na mikakati madhubuti ya kuwajengea uwezo wanawake kuwa viongozi kwa kueleza mafanikio na changamoto zinazowakabili.
Alieleza kuwa utafiti huo ulihusiasha magazeti ya Zanzibar Leo, Mwananchi, televisheni ya Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC TV), Zanzibar Cable (ZCTV) na mitandao ya kijamii ya Pemba Today na KTV, vyote viliripoti kwa chini ya asilimia 50 ya hyabari na vipindi vilivyohusisha wanawake ikilinganishwa na wanaume.
Aliongeza kuwa hali kama hiyo imehitokeza katika vyombo vyengine huku habari kuhusu wanawake viongozi zikipewa uzito mdogo.
Awali akifungua mkutano huo ulioshirikisha waandishi na wahariri wa habari, Mkurugenzi wa TAMWA Zanzibar, Dk. Mzuri Issa Ali, alieleza kuwa utafiti huo umelenga kuonesha namna vyombo vya habari vinavyomuangalia mwanamke.
Alisema matokeo ya utafiti huo yakitumia vizuri, yataimarisha utekelezaji wa kazi za vyombo hivyo lakini pia kutanua wigo wa utoaji na upatoikanaji wa habari zinazowahusu wanawake kupitia vyombo vya habari.
Aliongeza kuwa utafiti huo ni utekelezaji wa mradi wa ushirikishaji wanawake katika uongozi ambao unalenga kuwashajihisha wanawake kusimama na kuwania nafasi za uongozi katika uchaguzi mkuu ujao kupitia vyama vyao.
Nao baadhi ya washiriki wa mkutano huo, waliahidi kutumia matokeo ya utafiti huo kubadilisha mwenendo wa utoaji wa habari kwenye vyombo vyao ili kufanikisha malengo ya usawa wa kijinsia.