NA MWAJUMA JUMA

WAANDISHI wa habari nchini wameelezwa kwamba ni wadau wakuu wa kuhakikisha wanahamasisha jamii juu ya kupata chanjo ya corona na kujikinga.

Hayo yameelezwa na ofisa Mawasiliano kutoka Ofisi ya Katibu Mkuu wa wizara ya Afya Tanzania bara, Said Makora katika mkutano wa majadiliano juu ya ushirikiano baina ya serikali na vyombo vya habari ulioandaliwa kwa mtandao na Internews, kupitia mradi wa Boresha Habari.

Alisema kwamba Serikali wamekuwa waihamasisha sana watu wachanje chanjo hiyo ili kufikia angalau asilimia 60 ya watu wote waliochanjwa kama zilivyo nchi za wenzao.

“Sisi tunafanya hili lakini nyinyi waandishi wa habari ndio wadau waubwa sana kuhakikisha munatoa taarifa sahihi katika jamii kuhusu elimu hiyo ya Corona 19”, alisema.

Alisema katika utoaji wa taarifa zao wamekuwa waiwatumia maafisa wa habari, vyama vya habari pamoja na waandishi wenyewe ili kuona kwa namna gani wanafanikiwa.

Aidha alisema kwamba dhana ya Wizara ya Afya ni kulinda afya za wananchi wake na sambamba na kutoa taarifa kwa jamii kuhusu mwenendo, kujikinga na maelekezo juu ya afya zao.

“Serikali haina kitu cha kuficha katika hili, na tayari tumeshawafahamisha wakuu wote waliopo katika vituo wao ni wasemaji, sasa kama kuna kiongozi anakataa kutoa taarifa huyo anafanya kwa matakwa yake na sio kama hajapewa ruhusa ya kufanya hivyo”, alisema.