CAIRO, Misri
KOCHA Mkuu wa Al Ahly, Pitso Mosimane na timu yake wamepigwa faini na uongozi wa klabu kufuatia kichapo cha kushangaza cha miamba hiyo ya Cairo dhidi ya El Geish katika fainali ya SuperCup.

Ahly walikuwa wakitarajia kutwaa SuperCup kwa msimu wa 2020/21 baada ya kukosa ubingwa wa Ligi Kuu ya Misri mwezi uliopita ambao walipoteza kwa wapinzani wao, Zamalek. Lakini ilipokea kichapo panalti 3-2 mbele ya El Geish.

Vijana wa Mosimane walijikuta wakiwa na wakati mgumu kwenye mchezo huo baada ya kuzimaliza dakika kwa sare ya 0-0 kwenye Uwanja wa Borg El Arab huko Alexandria.
Matokeo yalikuwa ya kushangaza kwani hly, walikuwa wakipewa nafasi kubwa ya kutwaa kombe hilo kwa mara ya 12, lakini, walishangazwa na El Geish ambayo imeshinda Kombe lao la kwanza katika historia ya klabu.

Bila ya kupoteza muda, Ahly ilitoa taarifa ikisema kwamba Mahmoud El Khatib, rais wa klabu hiyo, ameamua kuwatoza faini ya EGP 300k wachezaji, mkurugenzi wa soka na benchi la ufundi baada ya kiwango kibaya kwenye mechi hiyo.

Kocha Mosimane amepigwa faini ya pauni 300,000 za Misri sawa na shilingi milioni 44. Ahly watakuwa kwenye presha watakapovaana na ENPPI FC katika mchezo wa raundi ya 16 ya Kombe la Misri iliyopangwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Alexandria leo.

Raia huyo wa Afrika Kusini ameshinda mataji mawili ya Ligi ya Mabingwa Afrika, CAF Super Cup, Kombe la Misri na SuperCup ya Misri tangu alipojiunga na klabu hiyo mnamo Oktoba 2020.