NA LUTFIA CHUM, MUM

WATU 18 wanashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kukutwa na matumizi ya dawa za kulevya katika mkoa wa Mjini Magharibi.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mwembemadema mjini Unguja, Kamanda wa polisi mkoani, Kamishna Msaidizi, Awadhi Juma Haji, alisema watuhumiwa hao walipatikana maeneo tofauti ya mkoa wa Mjini Magharibi.

Alieleza kuwa katika kipindi cha kuanzia Septemba 1 hadi 6 mwaka huu, polisi wakiwa katika operesheni za kuwasaka watu wanaojihusisha na uuzaji na utumiaji wa dawa hizo waliwakamata watu hao na kuwashikilia wakati wakikamilisha taratibu za kuwafikisha mahakamani.

“Tumefanikiwa kuwakamata watu 18 kwa tuhuma za dawa za kulevya na vitendo vyengine vya kihalifu ikiwemo kero na usumbufu katika jamii katika maeneo mbali mbali ya mkoa wetu,” Kamanda Awadhi alisema.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni John Nikodem Kasto (22) mkaazi wa Mtendeni, Salehe Khamis Hemed (26) wa Shaurimoyo, Yussuf Khamis Mbarouk (19) wa Mwanakwerekwe, Alawi Abdalla Khamis (19) wa Amani.

Wengine ni mkaazi wa Makadara, Yussuf Ramadhan Khamis (22), Nuru Salum Omar (21) mkaazi wa Nyerere, Hababa Shaaban Bokida (43) mkaazi wa Kiembesamaki, Shaaban Nassor Kigola (31) mkaazi wa Kiembesamaki pamoja na Zaid Ali Juma (42) mkaazi wa Uzi Tomondo.

Aidha Kamanda Awadhi aliendelea kuwataja watuhumiwa hao, Ahmada Said Chande miaka 31 mkaazi wa Kiembesamaki, Abdalla Salum Katema miaka 30 mkaazi wa Magomeni, Masoud Emanuel Maganga miaka 31 mkaazi wa Kiembesamaki,  Abdalla Hussein  Kibela miaka 38 mkaazi wa Kinuni.

Pamoja na hao kamanda Awadhi aliwataja watuhumiwa wengine kuwa ni wakaazi wa Kinuni, Kassimu Suleiman Vuai (19) na Soma Abdalla Abdalla (21), Adam Mohd Khatib (21) wa Kijitoupele, Khamis Vuai Ali (20) wa Amani na Yussuf Adam Saguda (50) mkaazi wa Kianga.

Akizungumzia uchunguzi wa makosa ya watuhumiwa hao, kamanda Awadhi alieleza kuwa unaendelea na kwamba watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria mara baada ya upelelezi  kukamilika  .