NA KAUTHAR ABDALLA

WADAU wa habari Zanzibar wameiomba serikali kutoa uhuru zaidi kwa vyombo vya habari ili viripoti habari kwa uwazi na undani zaidi.

Rai hiyo imetolewa na wadauu hao wakati wa mdahalo kuhusu uhuru wa kujieleza na maadili ya uandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa Kitengo cha uzazi shirikishi, Kidongochekundu Zanzibar.

Akiwasilisha mada ya maendeleo ya uhuru wa habari Zanzibar na changamoto zake, mtaalamu wa maswala ya habari kutoka shirika la internews, Ali Haji Mwadini alisema kuripotiwa kwa undani zaidi habari ndiko kutakopelekea kuibuka kwa changamoto zilizopo katika jamii.

Alisema katika uhuru wa habari kuna changamoto mbali mbali zinazopelekea kuongezeka kwa vitendo vya rushwa pamoja na udhalilishaji.

Pia alisema mbali ya changamoto hizo pia kuna tatizo la ukosefu wa haki za binaadamu kwa jamii kwani ndio waathirika wakuu wanaotokana na kutokuwa na uhuru wa kujieleza pamoja na vyombo vya habari kukosa uwazi wa kueleza mambo mengi.

Alisema tatizo linaonekana kwa baadhi ya vyombo vya habari ni kwamba uhuru wa habari upo kwa serikali pekee kwani ndio inayotoa taarifa za viongozi wa juu.

Mwandishi mwandamizi Salim Said Salim, akichangia mada katika mdahalo huo alisema licha ya kutokuwepo na uhuru mpana wa kujieleza katika vyombo vya habari lakini ni jambo la busara kwa waandishi wa habari kufuata miongopzo husika ya taaluma ya habari ili kulinda fani hiyo.

Alisema kufuatwa kwa kanuni na miiko ya fani hiyo ndio njia pekee itakayoleta ushindi katika suala la uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo habari nchini.

Alisema kuna baadhi ya habari zinakosekana katika taasisi za serikali kwa sababu ya viongozi wasio na uelewa wa fani ya habari kwani hujimilikisha ofisi na kupinga ushirikiano kati yake na vyombo vya habari.

Nae mwandishi mtangazaji wa kituo cha redi cha coconut fm, Amina Mchezo, alisema waandishi wengi wanakosa uhuru wa kufanya kazi kutokana sababu mbali mbali ikiwemo ya woga wa wamiliki wa vyombo wanavyfanyia kazi.