NA ASI MWALIM

WANANCHI na watumiaji wa mafuta ya taa, petroli na dizeli wameiomba serikali kudhibiti upandaji wa bei ya bidhaa hiyo ili kupunguza gharama za uendehaji wafanyabiashara wa vyombo vya usafiri na watumiaji binafsi wa bidhaa hiyo.

Wakizungumza na gazeti hili baadhi ya wanunuzi wa bidhaa hizo wakiwemo makondakta na madereva wa daladala na watumiaji wa vyombo vya moto walisema kupanda kwa bidhaa hizo kunasababisha kuongezeka kwa gharama za uendeshaji wa shughuli zao na maisha kwa ujumla.

Walisema jambo linalowapa hofu zaidi ni kuongezeka kwa bei kila mwezi hivyo wanaiomba Serikali kutafuta njia ya kuondoa tatizo hilo kwa kuweka bei angalu itakayotumika kwa muda wa miezi sita kama ilivyo kwa bidhaa nyengine.

Mmoja ya wadau hao ni Mohammed Rashid Mohammed mfanyakazi wa sheli ya Darajani, alisema kipindi kilichopita mafuta yalikua yanabadilishwa bei na kutumika zaidi ya miezi mitatu, lakini mwaka huu umekua tofauti kwani kila mwisho wa mwezi inatolewa bei elekezi mpya.

Alisema changamoto kubwa wanaipata kutoka kwa wateja wao kutokana na kutoizoea bei elekezi ambayo haidumu kwa muda mrefu, hivyo aliomba serikali kuangalia chanzo kinachosababisha bei kutumika kwa kipindi kifupi.

Alisema mara nyengine wanapata lawama kwa kusingiziwa tabia ya wizi au mashine zao mbovu kutokana na kiwango cha lita wanayotiliwa kwa mujibu wa pesa wanayoitoa na uzoefu wa lita wanazopata.

Nae Malik Sultan kutoka sheli ya Kisauni alisema wao si wahusika wa kupandisha wala kushusha bei lakini lawama za wateja zinafika kwao, kuwapawa ugumu kwa namna fulani hasa siku za mwanzo wa mwezi, hivyo aliomba serikali kueka kiwango kitakachotumika miezi sita ya mwanzo na miezi sita ya mwisho ili kutoa bei elekezi mbili tu kwa mwaka mmoja.

Alisema mara nyingi wateja hasa wa vyombo vya umma wanahisi wahudumu ndio wanafanya hitilafu kwenye mafuta na kushusha lawama kwao ingawa bei elekezi zinatolewa na kutangazwa na mamlaka iliyopowa dhamana.

Uhaba wa mafuta tunayopata kulingana na pesa tunayotoa unasababisha kushindwa kukamilisha ruti na kushusha abiria njiani jambo ambalo ni kujiondolea hadhi kwa abiria wako.

Dereva wa gari ya Mangapwani, Khamis Mohammed, alisema jambo linaloshangaza kuwa takriban biashara zote zinazofanywa Zanzibar zinatoka nje ya Zanzibar kwa nini bei ya mafuta haishuki wakati bidhaa zote zinashuka wakati zinatumia bandari hiyo hiyo.

Alisema kupanda mafuta kunasitisha baadhi ya shughuli zao na kurudisha nyuma uchumi wao kwani askari wahataki kuzidisha abiria hata mmoja ingawa mafuta yanaendelea kupanda siku hadi siku.

“Inatuumiza sana madereva wa gari za shamba tunapokwenda sheli zamani tunatia mafuta ya 60,000 lakini sasa hivi kama hujatia mafuta ya 90,000 gari haijajaa kwani bei inapanda laikini nauli ileile,” alisema.