NA SABIHA KEIS, WAMM

WAFANYAKAZI wa Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi wametakiwa kushajihika na kujiunga na Mfuko wa Taifa ya Bima ya afya (NHIF) ili waweze kupata huduma bora za afya   kwa uahisi na uhakika zaidi.

Afisa madai kutoka mfuko huo, Daniel Luttu alisema hayo katika ukumbi wa Wizara hiyo Maisara  alipokuwa akitoa elimu kwa wafanyakazi hao kuhusiana na umuhimu wa kujiunga na bima ya afya kwa wafanyakazi wa serikali.

Alifahamisha kuwa wafanyakazi wengi  hushindwa kumudu gharama za matibabu hivyo njia pekee za kumudu gharama hizo  wanapopatwa na maradhi ni kuwa na bima ya afya.

“mfanayakazi anapojiunga na mpango wa bima ya afya humuwezesha kumudu gharama hizo kwa kutumia kadi yake akishasajiliwa na kuwa mwanachama  halisi wa mfuko,” alieleza.

Alifahamisha kuwa ili kuona mfuko huo unatanua wigo na kuwanufaisha wananchi wote,  mfuko umeamua kutoa elimu kupitia taasisi za serikali ili kuwapatia huduma bora wafanyakazi nchini.

Aidha Luttu alisema kuwa taasisi nyingi za serikali zimeshajiunga na mfuko huo hivyo aliwasisitiza wafanyakzi hao kuwa na mwamko wa kuchangia matibabu yao kwa kujiunga ili  kupata matibabu bila ya usumbufu.

Akizungumzia faida ambazo mwanachama anazipata mara baada ya kujiunga na mfuko huo, Afisa huyo alisema kuwa mwanachama atamudu gharama zote za matibabu kupitia kadi atakayopewa.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Utumishi na Uendeshaji wa wizara hiyo,  Afisa Uhusiano wa Wizara, Yussuf Ali Khatib aliwashukuru viongozi wa NHIF ofisi ya Zanzibar kwa kwa kuwapatia elimu hiyo.

Aidha aliwataka wafanyakazi wenziwe kujiunga na hika na kuomba mfuko huo kuweza kuwapatia elimu zaidi kuhusiana na bima ya afya ya NHIF kila wanapopata nafasi.