NA TATU MAKAME
MKUU wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Ayoub Mohamed Mahmoud amewahimiza masheha wa mkoa huo kushirikiana na watendaji wa Idara ya uhamiaji kuwatambua wahamiaji haramu ili kuimarisha ulinzi na usalaama ndani ya mkoa.
Akizungumza katika semina kwa masheha wa mkoa wa Kaskazini huko Mkokotoni, Ayuob alisema kuna taarifa za kuwepo kwa wahamiaji haramu wanaofanya shughuli za kiuchumi na kuishi bila ya kufuata sheria za uhamiaji ndani ya mkoa bila kuwepo taarifa za watu hao.
Hivyo aliwataka masheha kuwatafuta watu hao na kutoa taarifa za watu wanaoingia ndani ya mkoa huo katika ofisi za uhamiaji ili kuchukuliwa za kisheria.
Alisema kwa kila shehia kuna wajumbe wanaomsaidia sheha lakini wanashindwa kuwatambua watu wanaoingia na kuwatoe taarifa ofisi husika.
Alisema wajumbe hao kushindwa kutoa taarifa kwa ofisi za uhamiaji ndani ya shehia zao miongoni mwa upungufu wa uwajibikaji kwa sheha hivyo elimu waliyoipata itawasaidia wao na wasaidizi wao kuwabaini wahamiaji haramu ndani ya shehia zao.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhamiaji Zanzibar, Mussa Masoud Haji akizungumza kwa niaba ya Kamishna Mkuu wa Idara ya uhamiaji Zanzibar, alisema utoaji wa elimu ya uhamiaji ni mwendelezo wa mafunzo yaliyoratibiwa na idara ya uhamiaji Zanzibar yenye lengo la kuwajengea uwezo masheha wa kutambua masuala ya uhamiaji ili kuimarisha usalama wa nchi.
Nao masheha walisema wahamiaji haramu wanaingia kupitia bandari bubu hivyo elimu hiyo itawasaidia kutekeleza wajibu wao wa kuwabaini wahamiaji hao.