BERLIN, UJERUMANI

MAJADALA wa wizi wa tafiti za kisayansi katika vitabu vilivyoandikwa na wagombea watatu wa Ukansela wa Ujerumani umepamba moto katika siku hizi za mwishoni mwa kampeni za uchaguzi nchini humo.

Kiongozi wa chama cha Kansela wa sasa wa Ujerumani ambaye anawania kurithi nafasi Angela Merkel,Armin Laschet kutoka chama cha Christian Democratic Union of Germany ni miongoni mwa wanaotuhumiwa kuiba kazi za waandishi wengine katika kitabu chake cha “Die Aufstiegsrepublik”.

Awali kulifichuliwa wizi wa kazi za kisayansi za watu wengine katika kitabu kilichoandikwa na mgombea wa ukansela wa Ujerumani kutoka Chama cha Kijani,Annale na Baerbock.

Wanasiasa hao wawili walikiri makosa yao ya kuiba kazi za waandishi wengine.

Mgombea mwengine wa ukansela wa Ujerumani anayetuhumiwa kuiba kazi za waandishi wengine katika kitabu chake ni Olaf Scholz kutoka chama cha Social Democrats (SPD).

Kabla yake,aliyekuwa Waziri wa Masuala ya Familia wa Ujerumani,Franziska Giffey alilazimika kujiuzulu kutokana na kupatikana na hatia ya kuiba tasnifu ya shahada yake ya uzamifu

Uchaguzi wa Bunge la Ujerumani uliopangwa kufanyika tarehe 26 mwezi huu wa Septemba.

Ujerumani inatarajia kushudia kipindi na awamu mpya baada ya Kansela Angela Merkel kutangaza kuwa atang’atuka madarakani. Merkel ameiongoza Ujerumani kwa awamu na vipindi vinne mfululizo na kubakia katika nafasi hiyo muda mrefu zaidi kuliko mwanasiasa yoyote mwingine wa Ujerumani.