TOKYO, JAPANI

WAGOMBEA wanne nchini Japani wanawania uongozi wa chama kikuu tawala cha Liberal Democratic, LDP na kimsingi, uongozi wa nchi hiyo.

Waziri Mkuu Suga Yoshihide amejiondoa kwenye kinyang’anyiro hicho na matokeo yake hayajulikani.

Wagombea waliojitosa rasmi kwenye uchaguzi huo ni Kono Taro ambaye kwa sasa ni Waziri anayesimamia Mabadiliko na aliyekuwa mwenyekiti wa Baraza la Utafiti wa Sera la LDP, Kishida Fumio.

Wengine ni aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Mawasiliano, Takaichi Sanae pamoja na Kaimu Katibu Mkuu Mtendaji wa LDP, Noda Seiko.Ni mara ya kwanza kwa wagombea wawili wanawake kuwania wadhifa huo.

Kiini cha kampeni huenda kikawa hatua za kupambana na virusi vya korona, na namna ya kurejesha uchumi na mfumo wa afya katika hali bora.

Sera ya ulinzi na mambo ya nje pia inaweza kuwa kwenye ajenda.Kura zinazowaniwa ni 766. Nusu zitapigwa na wabunge wa LDP na nyengine 383 zitaamuliwa na wanachama na wafuasi zaidi ya milioni moja.

Jana wagombea hao walielezea sera zao katika makao makuu ya LDP wakati wa mkutano na wanahabari,uchaguzi wa kuamua mshindi utafanyika Septemba 29.