NAIROBI, KENYA

WAISLAMU nchini Kenya wameliomba Baraza Kuu la Waislamu nchini humo (SUPKEM) liingilie kati kuhusu uamuzi wa shirika la kutetea haki za Waislamu (MUHURI) wa kuajiri Mkurugenzi Mkuu anayedaiwa kuwa mtetezi wa wapenzi wa jinsia moja.

Katika barua iliyoandikwa kwa Mwenyekiti wa MUHURI, Khelef Khalifa, waumini wa dini ya Kiislamu walisema wamekerwa sana na hatua hiyo.

Sehemu ya barua hiyo inasema,“Sisi kama Waislamu wa Kaunti ya Mombasa na Kenya kwa jumla, tumehuzunishwa sana na hatua ya hivi majuzi ya kumwajiri Mkurugenzi Mkuu mpya katika MUHURI. Tunakashifu vikali uamuzi uliochukuliwa na bodi ya shirika hilo kumwajiri mtu anayeenda kinyume na maadili ya dini yetu.”

Walisema hawatokaa kimya na kukubali shirika linalotumia jina la Uislamu kuendeshwa kwa misingi ya itikadi ambazo zinaenda kinyume na mafundisho ya dini hiyo tukufu.

Hatua iliyochukuliwa inaonyesha wazi kwenda kinyume na mafunzo ya Kiislamu.

Waislamu hao walimtaka Khalifa abadilishe jina la MUHURI ili likome kuhusishwa na Uislamu,bila hilo wametishia kuitisha maandamano ili kukemea wazi mienendo ya shirika hilo la kutetea haki za binadamu.

Mapema mwezi huu, MUHURI ilitangaza kumwajiri Marie Ramtu kuwa mkurugenzi mkuu mpya.

Ramtu aliwahi kufanya kazi katika shirika la kutetea haki za binadamu la mtandao wa Taasisi ya Kitaifa ya Haki za Binadamu ya Afrika (NANHRI).

Aliwahi pia kuhudumu katika shirika la Church World Service, ambapo inasemekana alihudumu kulinda masilahi ya watu walio hatarini kudhulumiwa kingono au kijinsia.