NA ASYA HASSAN

SERIKALI ya Mapindizi Zanzibar (SMZ), imeombwa kuandaa mazingira mazuri yatakayowasaidia wajasiriamali wadogo kuingiza bidhaa zao katika maeneo ya kitalii.

Ombi hilo limetolewa na Ofisa muwezeshaji wanawake kiuchumi kutoka Chama cha Waandishi wa Habari wanawake Tanzanzania (TAMWA Zanzibar), Nairat Abdalla Ali, alipokuwa akizungumza na gazeti hili ofisini kwake Mwanakwerekwe.

Alisema wanawakewengi hivi sasa wamehamasika na kuzalisha bidhaa tofauti lakini changamoto kubwa inayowakabili ni upatikanaji wa masoko ya uhakika kwa ajili ya kuuzia bidhaa hizo.

Hata hivyo alitumia fursa hiyo kuiomba serikali kukaa na kuliangalia suala hilo kwa upana wake ili kuweka mikakati imara itakayowapa nafasi wajasiriamali hao kuingiza bidhaa zao katika maeneo mbalimbali ya kitalii.

Ofisa huyo alisema endapo serikali itaweka mazingira hayo itakuza uchumi wa visiwa hivi pamoja na kutengeneza fursa mpya za ajira kwa vijana wengi waliyopo nchini.

Alitaja baadhi ya maeneo hayo kuwa ni pamoja na maduka ya kuuzia bidhaa za kitalii, mahoteli na hata uwanja wa ndege ni vyema serikali kuandaa mazingira mazuri ili wajasiriamali hao wakapata nafasi ya kuuza bidhaa zao.

“Hatua hiyo itasaidia kuinua kipato kwa wajasiriamali hao na kuongeza mapato serikalini, fedha ambazo zitasaidia kuwatumikia wananchi wengi katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo,” alisema.

Aidha alifahamisha kwamba licha ya wao kuwapatia elimu, mitaji na kuwatafutia masoko katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kuuzia bidhaa zao lakini haijafikia lengo hivyo ni vyema na serikali kuweka mkono wake ili kufanikisha malengo ya wajasirimali hao.

Aidha aliiomba serikali kuendeleza kuwaamini wajasiriamali hao kutokana na kuwa na uwezo mkubwa wa kuzalisha na kusaidia kuchangia ukuwaji wa uchumi wa nchi, hivyo ni vyema kuwasaidia pamoja na kuwajengea mazingira mazuri ili waweze kukua kibiashara.