NA ABOUD MAHMOUD

WAJUMBE wa Baraza la Skuli ya Sheria Zanzibar wametakiwa kufanya kazi kwa mashirikiano na Mkuu wa Skuli hiyo ili mafanikio yanayokusudiwa yapatikane.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman, alitoa wito huo alipokuwa akizindua baraza la kwanza la Skuli ya Sheria Zanzibar (ZLS) katika ofisi za wizara, Mazizini Unguja.

Waziri Haroun alisema bila ya kuwepo kwa mashirikiano kati yao, mafanikio ambayo ndio jambo muhimu kwa wananchi na taifa kwa ujumla hayawezi kupatikana.

“Nakuombeni wajumbe kuwa na mashirikiano ya pamoja kati yenu na mkuu wa skuli ya sheria ili lile lengo na dhamira tulizokusudia ziweze kufikiwa kwa maendeleo ya taifa letu,” alisema.

Haroun alisema baraza hilo limepata wajumbe wanaoendana na mkuu wa skuli hiyo hivyo ana matumaini makubwa kwamba kila kitu kitaenda kama kilivyopangwa na kufanikiwa kwa muda muafaka.

Aidha Haroun alisema anatarajia mwezi Oktoba, mwaka huu jengo jipya la Mahakama Kuu lililopo Tunguu litafunguliwa na kueleza kuwa wizara inajitahidi kuhakikisha kwamba majengo ya skuli ya sheria yanajengwa na kumalizika mwakani.

Sambamba na hayo Haroun alisema kuanzishwa kwa skuli hiyo kutawasaidia wanafunzi wanaosomea fani hiyo kufanya kazi kwa misingi na maadili ya kazi yao katika kuwasaidia wananchi.

“Maadili ni jambo muhimu sana katika sehemu yoyote, ikiwa nyumbani au kazini, hivyo kuanzishwa kwa skuli hii kutasaidia wanasheria wetu, mahakimu na majaji kufanya kazi kwa misingi ya maadili”, alisema.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Skuli ya Sheria, Jaji Mbarouk Salim Mbarouk, alisema baada ya kuanzishwa kwa skuli hiyo Zanzibar itakua miongoni mwa nchi za kupigiwa mfano katika fani ya sheria.

Jaji Mbarouk ambae pia ni Jaji Mstaafu wa mahakama ya rufaa Tanzania ameipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kwa kuanzisha jambo hilo ambalo ni muhimu kwa maendeleo ya nchi kwa ujumla.

“Nchi nyingi zina utaratibu wa kuanzisha skuli ya sheria kwa madhumuni ya kuendesha taratibu zile ambazo wanasheria wanazifanyia kazi, sisi tumechelewa kuanzisha kwa skuli ya sheria lakini tutachukua mazuri yote yaliyofanywa na wenzetu ili kufanya kitu ambacho kitakuwa bora zaidi,” alisema.

Naye Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu, alisema mahakama ipo tayari kushirikiana na skuli hiyo ili kuweza kufikia malengo yaliyokusudiwa na kupatikana maendeleo kwa misingi na taratibu zake.

Baraza la kwanza la skuli ya sheria Zanzibar lililozinduliwa lina wajumbe watano akiwemo Profesa Mohammed Makame, Hanifa Ramadhan Said, Ibrahim Mzee Ibrahim, Fatma Saleh na Slim Abdullah.