NA KIJA ELIAS, ROMBO

WAJUMBE wa jumuiya za tawala za mikoa na serikali za Mitaa (ALAT) mkoa wa Kilimanjaro, wameeleza kuridhishwa na ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Rombo kufuatia serikali kutoa shilingi bilioni 2.3 za ujenzi wa hospitali hiyo.

Akizungumza jana kwa niaba ya wajumbe wa jumuiya hiyo, mwenyekiti wa ALAT Mkoa wa Kilimanjaro, Salehe Mkwizu, alisema hatua hiyo ya serikali imelenga kuimarisha mazingira ya utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.

“Tumetembelea na kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali katika halmashauri ya wilaya ya Rombo, tunapongeza kwa usimamizi mzuri wa miradi hii, wamefanya kazi kubwa,”alisema Mkwizu.

Alisema ALAT mkoa wa Kilimanjaro inaipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kutoa fedha katika kusaidia ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika wilaya ya Rombo.

“Tumeelezwa kuwa serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, imetoa kiasi cha shilingi bilioni 2.3 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Rombo, ujenzi wa madarasa na barabara,”alisema.

Hata hivyo, Mkwizu alitoa wito kwa wakala wa barabara za vijijini na mjini (TARURA) mkoa wa Kilimanjaro kuhakikisha wanawashirikisha wananchi katika maeneo ya utelekezaji wa miradi ya miundombinu ya barabara ndani ya mkoa huo.

Alisema, “Tumewaagiza ndugu zetu wa TARURA wanapokuja kutekekeza miradi ya maendeleo ya barabara wahakikishe kwamba wana wanawashirikisha madiwani kwani wao ndiyo wanazijua barabara korofi zinafaa kupewa kipaumbele,”alisisitiza Mkwizu.

Nao baadhi ya Wajumbe wa ALAT Mkoa wa Kilimanjaro, kutoka wilaya za Same na Mwanga, walimsisitiza makandarasi wa barabara vijijini hususan ukanda wa milimani kufanyia kazi maeneo korofi ili kuziindoa changamoto zilizopo.

Naye diwani wa halmashauri ya wilaya ya Mwanga, Kiende Mvungi, alisema wapo wakandarasi ambao wamekuwa wakipewa tenda ya kutengeneza barabara na kwenda kutengeneza barabara ambazo ni rahisi na kuacha barabara korofi.