Wasafirisha marobota 324, doti 167 ya vitenge

NA LUTFIA CHUM (MUM)

WATU watatu wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa kutaka kumuhonga Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini, Awadh Juma Haji, baada ya kuwakamata wakisafirisha marobota ya vitenge 324 na doti 167, kwa njia ya magendo.

Akizungumza na Waandishi wa Habari huko ofisini kwake Mwembemadema Mjini Unguja, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini, Awadh Juma Haji, amesema watu hao walikamatwa wakisafirisha bidhaa hizo kwenda Tanzania bara, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Kamanda Awadh, alisema watu hao walikamatwa wakisafirisha bidhaa hizo katika maeneo ya Bandari bubu ya  Kisakasaka Wilaya ya Magharibi ‘B’ Unguja.

Kamanda  Awadh amewataja watuhumiwa hao ni Juma Mselem Ramadhan  mwenye umri wa miaka 29 ambae ni Fundi Ujenzi  mkaazi wa Kombeni Wilaya ya Magharibi ‘B’.

Wengine alisema ni  Othman Chema Yakoub  miaka 35  mkaazi wa  Dimani Wilaya ya Magharibi ‘B’ na Mahmoud Muhamed  Khatib  mwenye umri wa miaka 31 ambae ni wakala mkaazi wa Mtoni Kidato wilaya ya Magharibi ‘A’.

“Mara baada ya kukamatwa watuhumiwa hao wakishirikiana na mtuhumiwa anaetajwa kuwa mmiliki wa mzigo huo wa magendo walishawishi na kutoa rushwa ya shilingi milioni 2,000,000 kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi ili waweze kupewa mzigo wao” alisema Kamanda huyo.

Alisema tukio hilo la kushawishi na kutoa rushwa tayari wameshaliliripoti katika Mamlaka ya kupambana na Rushwa  ZAECA ili hatua za kisheria zichukuliwe kwa haraka.