NA LUTFIA CHUM {MUM}
WATU wawili wamekamatwa wakiwa na nyaraka bandia za serikali vikiwemo vyeti pamoja na mashine za kutengezea nyaraka hizo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Maghribi, Awadhi Juma Haij, aliyasema hayo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari huko ofisini kwake Mwembemadema Mjini Unguja.
Kamanda Awadh alisema watu hao wamekamatwa na askari wa JKU Agosti 25, 2021 majira ya saa 4:00 asubuhi , wakiwa na nyaraka hizo pamoja na mihuri mbali mbali ya serikali.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Hassan Fumu Simai miaka 50 , ambae ni mvuvi mkaazi wa Mtoni Mazurui na Shaaban Ali Suleiman mwenye miaka 50 mfanyabiashara mkaazi wa Mwanakwerekwe.
Aidha, Kamanda Awadhi amesema kuwa , chanzo cha kubaini tukio hilo ni mara baada ya waombaji wa ajira ya kazi ya kujiunga na Jeshi la Polisi Tanzania iliyotangazwa hivi karibuni katika kambi ya JKU na JKT.
Usajili huo, Kamanda Awadh alisema, Makao Makuu ya JKU walibainika kati ya waombaji hao walikuwa na vyeti feki, na baada ya kulifanyia kazi suala hilo walibaini kuwapo kwa mtandao uliojihusisha na vitendo hivyo.
Alisema katika kulifuatilia suala hilo pia walikamata mihuri 251, kutoka katika taasisi mbali mbali za serikali zenye nembo tofauti, ikiwemo mashine za Printer tatu, Laptop moja, Vyeti 271 vya kughushi na Vibati vya kugongea Mihuri ( stamp) sita vyote vikiwa vya kugushi .
Kamanda Awadhi amesema, watuhumiwa hao mara baada ya kukamatwa walikabidhiwa kwa Jeshi la Polisi mkoa wa Mjini Maghribi, kwa hatua zaidi za kisheria na watafikishwa mahakamani upelelezi utakapo kamilika .
Wakati huo huo, katika operesheni hiyo, wamefanikiwa kukamata watu wawili wakijihusha na kufanya biashara ya dawa za kulevya kwa kuuza na kutumia dawa hizo.
Tukio hilo alisema lilitokea Agosti 30, 2021, majira ya saa 7: 00 mchana huko Mahonda, askari walimkamata Michael Willbert John miaka 30 mkaazi wa Mahonda, akiwa ma kete 560 za dawa za kulevya aina ya Heroin, akiwa amezificha ndani ya Choo katika nyumba yake anayoishi.
Aidha, Kamanda Awadhi amesema, katika siku hiyo majira ya saa 4:00 asubuhi huko Kwaalinato Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Maghribi, askari walifanikiwa kumkamata Asya Abdalla Juma, mwenye miaka 21, akiwa na Dawa za kulevya aina ya Heroin Gram 20 jambo ambalo ni kosa kisheria.