NAIROBI, KENYA
WAENDESHAJI magari kutoka kaunti za Bungoma na Busia sasa wanamiminika nchini Uganda kununua mafuta ya bei rahisi kufuatia kupanda kwa bei nchini Kenya.
Uganda inauza bidhaa nyingi za mafuta kwa bei ya chini kuliko Kenya. Petroli inauzwa kwa Sh110 kwa lita, Sh30 chini kuliko ilivyo katika vituo vingi vya mafuta katika kaunti ya Busia.
Tofauti na Kenya, Uganda haina wakala wa kudhibiti bei ya mafuta.Udhibiti wa bei uliingizwa nchini Kenya kulinda wateja kutoka bei kubwa ambayo ilitozwa na mashirika ya kimataifa ya mafuta.
Vituo vya mafuta katika upande wa Uganda wa Busia na Malaba vilifurika watu kutoka Kenya.
Uganda hata hivyo, ni nchi isiyokuwa na bandari ambayo huingiza mafuta mengi kupitia Bandari ya Mombasa.
Kuingiza mafuta kupitia Kenya, Uganda inapaswa kulipa ushuru wa bandari kabla ya kupata tozo za uchukuzi kwa barabara au bomba kwa zaidi ya kilomita 1,165 kupitia mpaka wa Malaba au Busia.
Peter Odeke, mhudumu wa pampu katika mpaka wa Malaba na Uganda, alisema tangu kutangazwa kwa bei ya mafuta nchini Kenya, ameona utitiri wa magari yenye nambari za usajili za Kenya.”Magari mengi yenye nambari za usajili za Kenya yanajaza mizinga yao na kutoka jana wamekuwa wateja wetu wakuu,” alisema.