NAIROBI, KENYA

SERIKALI ya Kenya imetangaza kuwapiga marufuku raia wa nchi hiyo kwenda kufanya kazi za ndani nchini Saudi Arabia baada ya kuongezeka visa vya unyanyasaji na vifo vya kutatanisha vya Wakenya katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Wakenya wapatao 89 walipoteza maisha nchini Saudi Arabia katika kipindi cha miaka miwili iliyopita katika mazingira ya kutatanisha, hatua ambayo ilifanya serikali ya Kenya kusitisha kwa muda raia wake wanaokwenda kufanya kazi za ndani kwenda katika nchi hiyo ya Mashariki ya Kati.

Wiki iliyopita, Katibu katika Wizara ya Mambo ya Nje, Macharia Kamau, aliwaambia wabunge jijini Naiorbi kuwa, serikali ya Saudi Arabia inasema Wakenya hao walipoteza maisha kwa sababu ya matatizo ya moyo.

Hata hivyo sababu za vifo hivyo zinaendelea kuzua mashaka hata kwa maofisa wa juu wa Wizara ya Mambo ya Nje nchini Kenya, kuwa raia wake walipoteza maisha kwa sababu ya matatizo ya moyo.

Ilibainika kuwa tangu kuanza kwa mwaka huu, wakenya 41 wamepoteza maisha nchini Saudi Arabia na kutambuliwa na serikali jijini Riyadh.

Mwaka 2015 Serikali ya Kenya ilitia saini mkataba na serikali ya Saudi Arabia kutambua mawakala ambao wanaowasaidia raia wa Kenya wanaotaka kwenda kufanya kazi za ndani kwenda nchini humo, lakini kwanza kuwasilisha mikataba ya Wakenya hao kwenye Wizara ya Kazi.

Licha ya simulizi za kutatua madhila wanayopitia wakiwa huko Saudi Arabia, hivi karibuni maelfu ya Wakenya waliripotiwa kukwama Nairobi wakilalamikia kuchelewa kupata tiketi ya ndege kwenda kufanyia kazi Uarabuni.