NA MARYAM HASSAN

WAKILI wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Safia Serembe amepinga kuondolewa shitaka la mshitakiwa Kheri Hassa Aour (36) mkaazi wa Jambiani kwa madai kuwa bado wanao uwezo wa kuleta shahidi.

Pingamizi hizo alizitoa mbele ya Hakimu wa mahakama ya mkoa Mwera, Khamis Ali Simai, wakati shauri hilo lilipofikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kusikilizwa ushahidi.

Wakili huyo alisema shahidi waliyemtegemea ni daktari lakini yupo likizo na hawawezi kumlazimisha kufika mahakamani hapo ikiwa suala hilo lipo kisheria.

Hoja hizo ziliibuka baada ya wakili wa utetezi wa mshitakiwa huyo, Abdi Mzee, kuiomba mahakama kuliondoa shauri hilo kwa kuwa ni la muda mrefu na hakuna shahidi.

Alisema likizo aliyonayo shahidi huyo ni ya kisheria, hivyo aliiomba mahakama kuahirisha shauri hilo na kupanga tarehe nyengine kwa ajili ya kusikilizwa ushahidi.

Pia aliiomba mahakama kupuuzia ombi la wakili huyo kwa kuwa suala la likizo lipo kisheria kwa kila mfanyakazi.

Hakimu Khamis alisema baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote mbili mahakama imeona kuwa likizo ni haki ya msingi kwa kila mtu, hivyo si vyema kuondolewa kwa shauri kwa sababu shahidi yupo likizo.

Aliamua kuahirisha shauri hilo hadi Oktoba 4 mwaka huu na mshitakiwa amepelekwa rumande.

Mshitakiwa anatuhumiwa kwa kosa la kubaka alilodaiwa kutenda Febuari 8, mwaka jana majira ya saa 5:00 za usiku huko Jambiani wilaya ya Kusini mkoa wa Kusini Unguja.

Bila ya halali na kwa makusudi alimuingilia mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 14, ambae hajaolewa kitendo ambacho ni kosa kisheria.