NA KHAMISUU ABDALLAH

WALIMU wanaosomesha masomo ya utalii wameshauriwa kuwapa taaluma wanafunzi inayohitajika katika sekta hiyo, ili kuwawezesha kuajiriwa na kuleta mageuzi nchini.

Katibu Mkuu Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale, Fatma Mabrouk Khamis, alitoa kauli hiyo wakati akizungumza katika kikao kilichowashirikisha wadau wa utalii katika ofisi za Wizara hiyo Kikwajuni.

Alisema, kuna upungufu mkubwa katika mahitaji ya sekta binafsi katika suala la ajira kutokana na wanafunzi taaluma walizonazo ni tofauti na mahitaji yanayohitajika katika sekta yenyewe.

Aidha, alibainisha kwamba katika vyuo vya mahoteli wanazalisha ajira kwa vijana ambao wanahitajika kuajiriwa lakin katika sekta binafsi za mahoteli wao viwango ambavyo wanahitaji katika vyuo bado hawafikii kiwango cha mahitaji.

“Lengo kuu la kikao ni kukaa na wadau wa utalii ili kuangalia changamoto zinazoibabili sekta hiyo kwenye upande wa taaluma ya utalii kutokana na kuwepo na upungufu mkubwa baina ya mahitaji ya sekta binafi kwenye swala zima la ajira pamoja na mahitaji yanayohitajika katika sekta yenyewe,” alibainisha.

Katibu Fatma, alisema ni tatizo linalojitokeza kwa wanafunzi kutofikia kiwango cha kuajiriwa kutokana na walimu wengi hawana taaluma za utalii, na hawajawahi kufanya kazi katika sekta hivyo.

Alibainisha kuwa, kuna upungufu mkubwa wazanzibari kuajiriwa kwenye sekta ya utalii kwani asilimia 60 ya waajiriwa wote kwenye sekta hiyo ni wageni kutoka nje ikiwemo Tanzania bara na nchi nyengine za Afrika.