NA HAFSA GOLO
SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Zanzibar, limetoa wito kwa walimu na watahaniwa watarajiwa wa kidatu cha nne kuongeza bidii ya kufundisha, kusoma na kuweka mazingira bora ya elimu ili kuimarisha ufaulu.
Katibu wa shirikisho hilo,Khamis Mwinyi Mohamed alitoa wito huo alipokua akizungumza na gazeti hili ofisini kwake Kikwajuni.
Alisema mitihani ya taifa kwa watahaniwa watarajiwa wa kidatu cha nne inakaribia hivyo ni vyema walimu kuhakikisha wanatimiza wajibu wao katika utekelezaji wa majukumu yao ya kazi ikiwemo kumaliza mitaala kwa muda sahihi, ili watahaniwa hao waweze kukabiliana na mitihani yao.
Aidha alisema utekelezaji wa hatua hiyo uwe sambamba na wanafunzi kuongeza juhudi za kufatilia masomo yao ipasavyo, ili kujiandaa vyema na zoezi hilo ambalo linamaslahi mapana ya maisha yao.
Alieleza kuwa ni vyema walimu kutambua mahitaji mapya ya kielimu yaliotokana na mwenendo wa kiuchumi Zanzibar ambao yatahitajia wataalamu wazalendo wa fani mbali mbali.
“Hivi sasa serikali inahitaji wataalamu wazalendo kutoka fani mbali mbali ambazo zitasaidia katika utekelezaji wa mahitaji mapya ya kiuchumi ikiwemo uchumi wa buluu, mafuta na gesi asilia na utalii”,alifafanua .
Aliongeza Katibu huyo maeneo hayo bado wataalamu wazalendo bado ni kidogo, hivyo ni vyema walimu wabuni mbuni na mazingira yatakayosaidia wanafunzi kusoma na kufaulu vyema katika masomo yanayohusiana na maeneo hayo.
Hata hivyo aliwasihi watahaniwa watarajiwa wa kidatu cha nne kufuata sheria za mitahani pamoja na kujiepusha na vitendo vya udanganyifu.