NA LAYLAT KHALFAN

WAZAZI na Walezi nchini wametakiwa kuendeleza mashirikiano ya pamoja na walimu wa skuli mbalimbali kwa lengo la kufanikisha azma ya wanafunzi kujifunza kivitendo na kuwajenga kuinua kiwango bora cha ufaulu.

Mkurugenzi wa Skuli ya Someni ngazi ya Awali na Msingi, Ramadhan Fatawi Issa, aliyasema hayo katika ziara maalum ya kimasomo iliwashirikisha wanafunzi hao kwa lengo la kujifunza na kuongeza ujuzi.

Alisema baadhi ya wazazi wamekuwa hawazipi kipaombele fursa kama hizo za kimasomo kwa madai kuwa wanaenda kucheza na kuharibu pesa bila ya kujua athari kubwa ambayo inaweza kujitokeza.

Alisema ili mwanafunzi afaulu vizuri masomo yake ni lazima afanyiwe ziara mbalimbali za kimasomo kwa kuwa zinamsaidia kuongeza ufahamu wa akali na kufikiria kwa makini pale anaposomeshwa darasani kinadharia.

“Sasa ni wakati wa walimu na wazazi kuelimika kwa kusubutu kuwaandalia safari kama hizi watoto, ili waweze  kujifunza kwa vitendo badala ya kusoma kwa nadharia pekee,kwani hali hii inawafanya wanafunzi wengi kufeli masomo yao”, alisema.

Aidha, Mkurugenzi Fatawi, alifahamisha kuwa pamoja na kuwa wanafunzi hao kufundishwa masomo yanayohusiana na historia hiyo, lakini pia ziara hiyo iliwasaidia kuona uhalisia wenyewe na kupelekea kujibu mitihani yao kwa kujiamini zaidi.

“Kutembea lile eneo ambalo hujalifikia katika maisha yako peke yake ni kusoma na kufaidika kwa pande zote mbili ikiwemo katika maisha halisi ya kijamii pale unapokuwa mitaani”, alisema Fatawi.