NA ASIA MWALIM

JUMLA ya Wanafunzi 35,725 wanatarajiwa kuripoti katika skuli mbalimbali za Zanzibar kwa ajili ya kuendelea na masomo ya elimu ya msingi.

Mkuu wa Divisheni Idara ya Elimu Mbadala na Watu wazima Waziri Rajab Hamza, alitaja idadi hiyo wakati wa kikao cha pamoja cha kujadili mradi wa kurejesha skuli watoto walioacha masomo kwa Wilaya ya Mjini, kilichofanyika Skuli ya Muungano Zanzibar.

Alisema wanafunzi hao walishindwa kuhudhuria vyema kupata masomo, hivyo watarudishwa kwa ajili ya kuendelea kusoma ili kupatiwa haki hiyo ya msingi.

Aidha, alisema wanafunzi walioandikishwa katika mradi huo ni kati ya umri wa miaka saba hadi 14 kwa upande wa Wilaya za Unguja na Pemba.

Mkuu huyo alisema kwa upande wa Wilaya ya Mjini wanafunzi 454 wanatarajiwa kuripoti skuli, ambapo kati yao wanawake 219 na wanaume ni 235.

Aidha, alisema zoezi hilo endelevu linatarajia kupokea idadi kubwa zaidi kutokana na kuendelea kuhamasisha zaidi, ili kuwapata watoto wengine waliokua hawajafikiwa na taarifa hiyo.

Alisema mradi wa kurejesha watoto skuli kuendelea na masomo umetokana na sensa iliyofanywa kipindi kilichopita kutathmini hali ya Elimu hapa nchini, ambayo iligundua watoto wengi wenye umri mdogo wamesitisha masomo yao.

Alifahamisha kuwa tahmini ya Serikali imeona haja ya kuanzisha mpango huo mkakati wa kurejesha watoto skuli, ili kupata taifa lenye wasomi.

Hata hivyo, aliwataka wazazi na walezi kuwa na mashirikiano ya karibu, ili kuliendeleza suala hilo kwa ushawishi ili kuacha kufanya shughuli za mitaani, ili kupata taifa lenye wasomi.

Ofisa Elimu Wilaya ya Mjini, Kibibi Mohammed Mbarouk, alisema mradi huo ni kutokana na kauli ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,  Dk. Hussein Ali Mwinyi, kutaka watoto wote walioacha masomo na walioshindwa kuandikishwa skuli warudishwe kuendelea na masomo kama watoto wengine.